ZUCHU APEWA UBALOZI WA SATURN CORPORATION, ATANGAZA KUIPIGANIA BIDHAA YA TANZANIA
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Zuchu, amesaini mkataba wa ubalozi na Kampuni ya Saturn Corporation LTD, inayojihusisha na uzalishaji wa magari nchini Tanzania, ikiwemo magari yenye chapa ya Howo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 20, 2026 jijini Dar es Salaam, Zuchu amesema amefurahishwa na nafasi hiyo kubwa ya kuwa balozi wa kampuni ya kizawa inayozalisha magari hapa nchini, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa pamoja na kuhamasisha Watanzania kupenda bidhaa zinazotengenezwa nchini.
“Mimi ni msanii ambaye napenda kuona Taifa langu na wawekezaji wa ndani wakikua kiuchumi. Kampuni hii inazalisha magari hapa hapa nchini, hivyo ni wajibu wetu sisi Watanzania kuzipenda na kuzithamini bidhaa za ndani,” amesema Zuchu.
Aidha, amesema uwepo wa kiwanda hicho kilichopo Kigamboni ni ishara nzuri ya maendeleo ya viwanda nchini na fursa kwa vijana wengi kupata ajira na kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Saturn Corporation LTD, Rehmatullah Habibi, amesema kampuni hiyo imefanikiwa kuajiri zaidi ya vijana 360, wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu ambao wamepewa mafunzo maalum ndani ya kiwanda hicho.
“Kiwanda chetu kina uwezo wa kuzalisha magari 30 kwa siku, na tunalenga kuzalisha magari zaidi ya 6,000 kwa mwaka kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji tuliyowekewa. Sambamba na hilo, tunaendelea kuwa walipakodi wazuri kwa Serikali yetu,” amesema Habibi.
Mbali na shughuli za uzalishaji wa magari, Habibi amesema kampuni hiyo pia ipo kwenye mazungumzo ya kudhamini klabu ya Coastal Union kama sehemu ya kuunga mkono sekta ya michezo na burudani nchini.
Aidha, amesema kampuni hiyo inatarajia kuzindua rasmi magari mapya aina ya Howo Pickup katika siku za hivi karibuni.


