JESHI LA POLISI PWANI LAKANUSHA TAARIFA ZA MIILI SITA KUOKOTWA MTO RUVU
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa miili ya watu sita imeokotwa ikielea katika Mto Ruvu, Wilaya ya Bagamoyo, likisisitiza kuwa taarifa hizo si za kweli.
Kwa mujibu wa Jeshi amesema Polisi, taarifa hiyo imekuwa ikisambazwa mara kwa mara katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram na Facebook licha ya kufanyiwa ufafanuzi mara kadhaa na mamlaka husika.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase amesema taarifa hiyo ilianza kusambazwa kwa mara ya kwanza Desemba 21, 2016 na kufafanuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz, kuwa haikuwa ya kweli.
Aidha, amesema taarifa hiyo ilijitokeza tena Septemba 13, 2025 katika mitandao ya kijamii na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilitoa ufafanuzi rasmi siku iliyofuata, Septemba 14, 2025, likikanusha taarifa hizo.
Hata hivyo, licha ya ufafanuzi huo kutolewa mara mbili, taarifa hizo zimeendelea kusambazwa tena kuanzia Juni 8, 2026, jambo ambalo limeibua taharuki kwa baadhi ya wananchi.
Jeshi la Polisi limesema hakuna tukio la kuokotwa kwa miili sita katika Mto Ruvu lililoripotiwa au kuthibitishwa na vyombo vya dola, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini na taarifa wanazozisoma au kuzisambaza kupitia mitandao ya kijamii.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa wito kwa jamii kupuuza taarifa hiyo na kuacha mara moja kusambaza taarifa zisizo za kweli ambazo zinaleta taharuki kwa jamii," imeeleza taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha taarifa hizo za uongo pamoja na watu wanaozisambaza, huku likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika.
Aidha limewakumbusha wananchi umuhimu wa kuthibitisha taarifa kutoka katika vyanzo rasmi kabla ya kuzisambaza ili kuepusha upotoshaji na taharuki isiyo ya lazima katika jamii.

