"LIWE JUA IWE MVUA MIRADI YA REGROW IKAMILIKE" CP. WAKULYAMBA



Na Mwandishi wetu 

Wakandarasi wote wanaotekeleza Miradi ya  chini ya mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Nyanda za juu Kusini (REGROW)   wametakiwa kuhakikisha wanajipanga vyema kufanya kazi katika misimu yote iwe ya jua au mvua ili kuikamilisha kwa wakati uliopangwa.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu  Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna  Benedict Wakulyamba,  Mkoani Morogoro alipotembelea na kukagua miradi ya REGROW inayotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Nyerere .

Kamishna Wakulyamba licha ya kuridhishwa na kasi ya utekelezwaji wa miradi hiyo, amesema uongozi wa Wizara hiyo hautopenda kuona miradi inasuasua kwa sababu zinazoweza  kuzuilika mapema, hivyo wakandarasi wajiandae vyema kufanya kazi bila kukwamishwa hata na mvua zitakazonyesha hapo baadae.

Aidha Kamishna Wakulyamba amewaahidi Wakandarasi hao kuwa uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Mhe. Waziri, Angellah Kairuki (Mb) utaendelea kutoa ushirikiano wakati wote na kuwa milango ipo wazi iwapo wanajambo la kupata uwelewa wa pamoja.

Kamishna Wakulyamba ameendelea kutoa rai kwa wananchi kuilinda miradi hiyo ili iwe baraka ya maendeleo ya kiuchumi nchini na kwa yeyote atakae ifanyia hujma atashughulikiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria.

Akiwa katika Bwawa la kuzalisha Umeme la  Mwalimu Nyerere na baada ya kujionea ujenzi unaoendelea, Kamishna Wakulyamba amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji, na Misitu, huku akiagiza Maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi kuhakikisha ulinzi wa rasilimali hizo unaimarika. 

Amesema mradi  wa REGROW  kwa kushirikiana na Wadau unatekeleza Mradi wa umwagiliaji Madibira na ufukuaji wa mikondo ya mito Mbarali ili maji yakutosha yapatikane kwa matumizi ya Ikolojia na Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Ruaha na kisha kwenye Bwawa la Mwl Nyerere.

Naye Naibu kamishna wa uhifadhi na maendeleo ya biashara Herman Bathiho ameleza ujenzi unaoendelea ni pamoja na Ujenzi wa Jengo la Abiria,  Kiwanja cha Ndege cha Mtemere, lango la kuingilia na kutoka la Mtemere,  Nyumba za Watumishi na kuahidi kuwa TANAPA itaendelea kusimamia vyema utekelezaji wa miradi hiyo.

Powered by Blogger.