RAIS WA UJERUMANI KUTEMBELEA MAKUMBUSHO YA VITA VYA MAJIMAJI, SONGEA


Na Mwandishi Wetu- Songea

Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujeruman Mhe. Dkt Frank Walter Steinmeier anatarajiwa kutembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya MajiMaji Songea kesho tarehe 1 Novemba 2023 kwa lengo la kutoa heshima kwa mashujaa wa vita hivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amesema maandalizi ya kuupokea ugeni huo yamekamilika ambapo baada ya kufika uwanja wa ndege wa Songea ataenda moja kwa moja katika Makumbusho ya Vita vya MajiMaji.

Amesema akiwa katika Makumbusho hiyo atapata historia ya makumbusho hiyo na kutoa heshima kwa mashujaa waliokufa katika vita hivyo vilivypiganwa mwaka 1905 mpaka 1907.

Kanali Thomas ameongeza kuwa pamoja na kutoa heshima kwa mashujaa wa Vita vya Majimaji Rais huyo wa Ujerumani  atakutana na baadhi ya wahanga wa vita hivyo na kisha kuelekea Shule ya Msingi MajiMaji.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamshna  Benard Wakulyamba amesema kuwa kwa upande wa Wizara ya Maliasili ikiwa ni pamoja na Makumbusho ya Taifa la Tanzania ambao ndio wasimamizi wa Makumbusho ya Vita vya MajiMaji maandalizi yamekamilika kwa ajili ya kumpokea Rais huyo wa Ujerumani.

Kamishna Benedict Wakulyamba, ameongeza kuwa ziara hiyo ya Rais wa Ujerumani katika Makumbusho ya Majimaji  licha ya kuimarisha mahusiano ya kimataifa pia itakuwa chachu ya kuongeza utalii nchini.

Powered by Blogger.