WATUMISHI 11 TAMISEMI,MANISPAA YA KIGOMA UJIJI WAPANDISHWA KIZIMBANI



Na Mwandishi wetu

Watumishi wa Ofisi ya Tamisemi na Manispaa ya Kigoma ujiji wamepandishwa kizimbani kwa kosa la uhujumu uchumi namba 3  ya mwaka 2023 yenye mashtaka 11 ikiwemo kosa la utakatishaji fedha kiasi cha Tsh Milioni  463.5  inayowahusu watumishi 11 wa Manispaa  hiyo na Ofisi hiyo ya Kigoma.

Akisoma mashtaka hayo jana mbele ya hakimu Mfawidhi wa Mahakama  ya wilaya ya hakimu mkazi Hassan Momba, Wakili mwandamizi wa serikali Anosisye Erasto ameieleza mahakama kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya juni 1, 2022 na Juni 5, 2023 katika Manispaa ya Kigoma ujiji na Jiji la Dodoma.
Baadhi ya mashitaka wanayoshitakiwa  watumishi hao ni pamoja na kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kugushi, matumizi mabaya ya madaraka, kutakatisha fedha, kuisababishia mamlaka ya serikali hasara.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma ujiji Athumani Msabila, watumishi wa ofisi ya Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa(Tamisemi) Dodoma Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira.

Wengine ni watumishi toka ofisi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Frednand Filimbi, Salum Juma, Moses Zahuye, Joel Shirima, Jema Mbilinyi, Kombe Kabichi, Frank Nguvumali na Bayaga Ntamasambilo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Katika kesi hiyo washitakiwa wanasimamiwa na mawakili wanne ambao ni Sadiki Aliki, Michael Mwangati, Eliutha Kvyiro na Victoria Nyembea.

Aidha washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutona na mahakama kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza mashauri yao ikiwemo shitaka la uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara.

Kesi hiyo imehairishwa hadi novemba 20 mwaka huu itakapotajwa tena kwaajili ya kutoa uamuzi wa dhamana kwa washitakiwa watano ambao hawahusiki na shitaka la utakatishaji fedha kama watakuwa na haki ya kupata dhamana.
Powered by Blogger.