TANROADS YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA BASHUNGWA LA KUTAFUTA SULUHISHO LA KUJAA MAJI MTANANA

Na Mwandishi wetu,Dodoma 

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), umerejesha mawasiliano ya barabara kuu ya Morogoro – Dodoma eneo la Mtanana iliyofungwa kwa saa kadhaa leo Januari 09, 2024 kufuatia maji kujaa katika eneo hilo na kupelekea kutopitika kwa muda.

Urejeshaji wa Mawasiliano ya barabara hiyo ni kufuatia agizo la Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alilotoa kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo kuhakikisha wanafungua Mawasiliano na kufanya tathimini ya kumaliza changamoto katika eneo hilo.

Akitoa taaarifa ya hali ya barabara, Mkurugenzi wa Idara ya Matengenezo TANROADS, Eng. Dkt. Christina Kayoza, amesema kuwa tayari magari yameruhusiwa kupita katika eneo hilo na timu ya Mameneja wa TANROADS kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro na Singida wapo katika eneo hilo kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama.



Kuhusu Suluhisho la Kudumu katika eneo hilo, Dkt. Kayoza ameeleza kuwa upembuzi yakinifu umefanyika katika eneo hilo ambapo sehemu ya barabara hiyo itanyanyuliwa juu na kujengwa madaraja yenye urefu wa mita tano ambayo yataruhusu maji kupita bila kuharibu barabara hiyo.

Aidha, TANROADS inaendelea kufanya matengenezo ya dharura katika eneo hilo pamoja na maeneo mengine nchini yaliyoathiriwa na mvua katika barabara kuu na barabara za mikoa nchini.

Powered by Blogger.