TANZANIA YANG'ARA HUDUMA ZA MAABARA AFRIKA

 



Na, WAF - DODOMA 

Tanzania  imekuwa nchi  ya tatu kwa ubora  wa Huduma  za maabara kati  ya nchi  56 za Bara la Afrika   kupata  ithabati ya ubora.

Hayo yameelezwa Naibu Waziri wa Afya, Dkt.  Godwin Mollel, leo Mei 24, 2024Jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji wa vyeti kwa maabara zilizopata idhibati ya Kimataifa.

"Tuna kila sababu ya kujipongeza  hili ni jambo kubwa, nawapongeza mmefanya jambo kubwa sisi kama Serikali tunajivunia ninyi wataalamu wa maabara," amesema Dkt. Mollel

Amesema anaamini  mwakani watakuwa nafasi ya kwanza, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amezidi kutoa fedha katika sekta ya afya ili wananchi waweze kupata Huduma bora na za wakika.


Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha watu wa maabara wanaendelea kuwa na maslahi na kuwataka wataalamu hao kujiamini na kufanya vizuri zaidi katika kutoa Huduma bora za maabara.

"Natoa rai kwa   wasimamizi wa Hospitali kuhakikisha wanawawezesha watu wa maabara, naombeni mnaofanya maamuzi kwenye eneo la maabara hili liangalieni hawa ni watu muhimu sana katika hospitali zetu nchini.

Aidha amewatia moyo wataalamu hao na kuwambia wasibweteke kwani Serikali chini ya Uongozi wa Rais Samia umewekeza vifaa na miundombinu ya kisasa ili mwananchi aweze kupata Huduma bora za afya.


Vile vile Dkt. Mollel ameagiza  vituo vya afya kutumia miongozo katika kuboresha huduma za maabara na serikali ya awamu ya sita ya  Dkt. Samia Suluhu Hassan  inaendelea kusimamia afua za uboreshaji wa huduma za afya nchini. 

"Hivyo nitoe rai kwa viongozi wote tuweze kusimamia kikamilifu vituo  ili vitumie miongozo yote iliyotolewa na Wizara ya Afya katika  kuboresha huduma zetu za Maabara nchini kwa ubora wenye kiwango cha kimataifa,"amesisitiza Dkt.  Mollel.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ubora na Uchunguzi wa Magonjwa na Matengenezo ya vifaa tiba, Dkt.  Alex Magesa amesema lengo la Mkutano huo ni kutoa  tuzo na vyeti kwa maabara zilizopata ithibati za kimataifa  kwa mwaka wa fedha 2023-2024.



Dkt. Magesa amesema wadau wa maabara wanashirikana katika kuboresha sekta ya maabara lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora na nzuri zinatolewa ambapo kwenye kuboresha huduma wamekuwa bega kwa bega na kutatua changamoto za wataalamu wa maabara nchini.

Ametaja   mafanikio yaliyopatikana mpaka Sasa ni  pamoja na kujenga uwezo wa  Maabara ya Taifa na kuweza kugundua magonjwa ya  milipuko kama kule Kagera.

"Maabara ya Taifa imekuwa kituo cha Kanda na haya ni mafanikio makubwa kwetu”, amesema Dkt. Magesa.

Amesema mpaka sawa wamefanikiwa  kufikia maabara 83 ambazo zimepata idhibati ya Kimataifa ambapo Hali hiyo  inaifanya Tanzania kuwa Nchi ya 3 yenye ithibati nyingi.

Amesema kupata  kupata Ithibati ni gharama kubwa hivyo wanaishukuru Serikali kwa kuweza kulisimamia uwekezaji katika upande wa maabara.


Mwisho

Powered by Blogger.