Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Alliance For Democract Change (ADC) Taifa Doyo Doyo ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Uenyekiti Taifa baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Hamad Rashid kumaliza muda wake kikatiba.
Akitangaza nia yake mbele ya waandishi wa habari jana Dar es Salaam amesema ameona anatosha kugombea nafasi hiyo na endapo atafanikiwa atapambana ili kuendelea kukiimarisha chama hicho kiweze kufikia viwango vya juu.
"Kutokana na uzoefu wa miaka 10 nilioupata kutoka kwa Mwenyekiti aliiyemaliza muda wake naahidi kuyaendeleza mazuri yote hususan kuilinda katiba ya chama chetu.
Amesema Juni 11 mwaka huu atachukua fomu rasmi kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo na kuwaomba wanachama wenzake ndani ya chama hicho itakapofika Juni 27 mwaka huu wamchague aweze kufanya yote aliyokusudia na chama kiweze kufikia viwango vya juu.
Hata hivyo katika mkutano huo Doyo alimshukuru Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwa kuilinda katiba ya chama aliyoitumikia kwa awamu mbili na kukubali kuachia ngazi huo ni mfano mzuri kwa kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa na tabia ya kun’gang’ania madaraka.
“Katika utaratibu huu Hamad Rashid ametufundisha jambo hususan sisi vyama vya Siasa na hili liwe somo kwa viongozi wengine kutoka vyama mbalimbali vya siasa "amesema Doyo.
Doyo ameongeza kuwa endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo atakisaidia chama kusukuma ajenda za upatikanaji wa ajira,elimu Bora,na kupata wabunge wawakilishi watakaowakilisha wananchi katika changamoto zao bungeni .
Naye, Mwenyekiti wa Vijana Taifa Ibrahimu Pogora amempongeza Doyo kwa kutangaza nia yake na kuahidi kushirikiana naye katika harakati zote za uchaguzi kupata wadhamini bara na visiwani
Hivyo aliwataka wanachama wa Chama hicho kutambua kuwa wanadhamana na mtia nia hiyo kwa kuwa yeye si mwanachama wa kuletwa bali ni mwanzilishi wa chama hicho.