MRADI WA KUBORESHA HUDUMA ZA MAWASILIANO WATARAJIWA KUANZA
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
Utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Huduma za Mawasiliano, utakaojumuisha Kata ya Bukiko, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, ili kuondoa tatizo la mawasiliano, unatarajiwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amebainisha hayo tarehe 7 Juni, 2024 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi.
Naibu Waziri Mahundi amesema, mradi huo utakaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote {UCSAF}, utahusisha kuongeza huduma za mawasiliano kwa teknolojia ya 3G na 4G, na kuimarisha miundombinu ya nishati, ikiwemo kuweka jenereta.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo kuhusu kukwamishwa kwa mradi huo uliotengewa fedha Mwaka wa Fedha 2022/2023, Naibu Waziri huyo amemhakikishia kuanza kwa mradi huo mwaka ujao wa fedha, na kwamba Serikali haijaukwamisha.
Aidha, Naibu Waziri Mahundi, amezitaka kampuni zote zilizopewa kazi za kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa minara, kuhakikisha zinatekeleza wajibu wake, kwani Serikali inataka kuona miradi hiyo inatekelezwa na kukamilika.
Majibu ya Naibu Waziri Mahundi yalitokana na swali la Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Patrick Ndakidemi, aliyetaka kufahamu sababu za Kampuni ya Tigo iliyoshinda zabuni ya kujenga mnara katika Kata ya Uru Himbwe, kukwama kutekeleza mradi huo.
Kuhusu Wananchi wa Kata ya Gehandu, Manyara, kutumia mnara wa mawasiliano wa Kata ya Ishiponga kama alivyouliza Mbunge wa Taifa Vijana, Asia Halamga, Naibu Waziri Mahundi amesema, Serikali inalifanyia kazi eneo hilo, kwanza kwa kuboresha mnara wa jirani, ili masafa yafike kwa uhakika Kata ya Gehandu, huku ikijipanga kujenga mnara wake katika kata hiyo.