DC SHAKA ATOA MAAGIZO MANNE KUTATUA KERO ZA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu 

KILOSA: MKUU wa Wilaya ya KIlosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka ametoa maagizo manne kuhakikisha wananchi katika Kijiji cha Kitete wilayani humo wanapata huduma bora.

Maagizo hayo ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kushirikiana na ofisi ya ardhi ya wilaya kufuatilia mchakato wa umilikishwaji wa shamba kwa mwekezaji katika kijiji hicho.

Pia, ameagiza wananchi washirikiane na viongozi kijijini hapo kuweka mikakati na kuanza mchakato wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Kitete.

Shaka ametoa maagizo hayo Julai 9, mwaka huu katika kijiji hicho alipofika na kufanya mkutano wa hadhara akiwa katika ziara ya kikazi akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya KIlosa.

Mkuu huyo wa wilaya alifikia kutoa maagizo hayo baada ya kupokea kero mbalimbali ikiwemo ya mwekezaji kukabidhiwa shamba bila ya kufuata utaratibu.

"TAKUKURU na ofisi ardhi Wilaya ya Kilosa fuatilieni kwa haraka mchakato wa umilikishwaji wa shamba hilo kwa mwekezaji huyo na majibu yaletwe ofisini kwangu," ameagiza.

Kuhusu zahanati, wananchi wa Kitete walilalamikia kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika maeneo mengine kwa kukosekana zahanati kijijini hapo.

"Nimelipokea suala hili nalichukua na kwenda kulifanyia kazi ikiwemo kuwashirikisha wadau mbalimbali ili mchakato wa ujenzi wa majengo ya zahanati yaanze mara moja kwa kushirikiana na mbunge wa KIlosa, Profesa Palamagamba Kabudi," amesema. 

Sambamba na hilo Shaka amewaomba viongozi na wananchi wa Kitete kujitokeza kushiriki ujenzi wa zahanati hiyo.

Aidha, Shaka amemtaka mkuu wa shule ya sekondari kijijini hapo kwa kushirikiana na ofisa ardhi wa wilaya kuhakikisha eneo la shule hiyo linatambulika na linapatiwa hati kwa haraka.

AAHIDI UMEME 

Shaka aliwaahidi wananchi kuwa hadi Septemba 30, mwaka huu umeme utakuwa umefikishwa kijijini hapo, hivyo Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kilosa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha hilo linatimia.


"Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anapambana usiku na mchana kuhakikisha anawaletea wananchi maendeleo na huduma za kijamii wakiwemo wananchi wa Kitete, hivyo mnapaswa kumuunga mkono kwa kuchapa kazi, kudumisha amani, Umoja na mshikamano," amesisitiza.

Powered by Blogger.