EWURA YAWATAKA WAWEKEZAJI WANAOTAKA KUFANYA SHUGHULI ZA UCHAKATAJI,USAFIRISHAJI NA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA KUOMBA KIBALI

 



Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaokusudia kufanya shughuli za Uchakataji,Usafirishaji na Usambazaji wa Gesi Asilia nchini kuhakikisha wanaomba na kupewa kibali cha ujenzi kabla ya kuanza kufanya shughuli hizo.

Haya yamesemwa jijini Dar es Salaam leo julai 7,2024 na Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA,Titus Kaguo wakati wa maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ''Sabasaba'' kwenye banda la mamlaka hiyo.

Amesema Kibali hicho cha ujenzi kwa waombaji kinatoka kwa mujibu wa sheria ya EWURA kwa mujibu wa kifungu cha 126 cha Sheria ya Petroli.''Mamlaka inajukumu la kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na chini wa gesi asilia zinazojumuisha uchakataji,usafirishaji,uhifadhi na usambazaji wa gesi asilia nchini,''amesema.

Kaguo amesema kuna aina mbalimbali ya vibali katika shughuli hizo za uchakataaji,usafirishaji na usambazaji wa gesi ikiwemo vibali vya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia katika sekta ndogo.


Akitaja aina hiyo ya vibali vya ujenzi ni pamoja na kibali cha ujenzi wa Kituo cha kuchakata gesi,Bomba la kusafirishia gesi,Bomba la Kusafirisha gesi ,Bomba la Usambazaji,Kituo cha kurejeshea gesi asilia kutoka kwenye hali ya kimiminika,Kituo cha uzalishaji gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG)kwenye Kituo Mama,Kituo cha kujaza gesi iliyoshindiliwa na Kituo cha Kujaza Gesi asilia Kimiminika (LNG).



Kaguo amesema utaratibu wa kuomba kibali hicho cha ujenzi uombwa kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa taarifa za leseni na uagizaji (LOIS)ambao unapatikana kupitia tovuti ya Mamlaka yao.

''Mwombaji wa kibali cha ujenzi wa miundombinu hiyo anatakiwa kuwa na taarifa sahihi ikiwemo Jina la Kisheria la Kampuni inayoomba (kwa kampuni),Anuani ya Kampuni,Mtu Mahsusi atakayewasiliana na EWURA kwa niaba ya Kampuni na nafasi yake katika Kampuni,Nakala za Vyeti vya Utambulisho Kampuni,Leseni ya Biashara pamoja na makubaliano ya ushirikiano (Memorandam of understanding/ Articles of Association.

''Pia mwombaji anapaswa kuwa na nambari ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), usajili wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT),ramani ya mradi utakapojengwa,mpango wa matumizi ya ardhi unaonisha kwamba eneo linaweza kutumika kwa shughuli za gesi asilia, Uthibitisho wa hati ya umiliki wa ardhi,Cheti cha tathmini ya athari ya mazingira (EIA),Nakala ya sera ya usalama ya kampuni pamoja na Barua ya ridhaa kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC.

Aidha amesema kwa mujibu wa kifungu cha 131 cha Sheria ya Petroli, mtu yeyote anayetarajia kufanya shughuli za uchakataji,usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia anapaswa kuwa na leseni iliyotolewa na EWURA.

Powered by Blogger.