KIJIJI CHAWAKATIA BIMA YA AFYA WAKAZI WAKE WOTE
LUDEWA
Wananchi 3,149 wa kijiji cha Mundindi kilichopo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wametengeneza historia ya kipekee baada ya Serikali ya kijiji hicho kuwakatia bima ya afya wanakijiji wote ili waweze kupata huduma ya afya bila kikwazo cha fedha.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kulipa fidia Sh15 bilioni ili kupisha miradi ya Liganga na Mchuchuma ambapo kijiji hicho kilikuwa na eneo katika eneo la mradi huo na kukiwezesha kupata fidia ya Sh464 milioni.
Kati ya fedha hizo, na Sh400 milioni kijiji kiliamua kununua hati fungani katika moja ya taasisi ya kifedha hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo Julai 12, 2024 na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundindi, Sapi Mlelwa wakati wa hafla ya kuwakabidhi kadi za bima ya afya wananchi hao, iliyofanyika kijijini hapo.
Amesema kiasi hicho cha Sh400 milioni walichonunua bondi ya hati fungani, kinawawezesha kijiji hicho chenye kaya 524, kupata gawio la Sh41 milioni kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
Amesema katika gawio la kwanza, wanakijiji walikubaliana kulipiana bima ya afya ambayo thamani yake ni Sh12.9 milioni.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kijiji hicho ni cha mfano kote nchini kwani viongozi wake wamefanya ubunifu mkubwa wa kuhakikisha afya za watu wao zinatunzwa.