WATUMISHI MVOMERO WAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KUHAMASISHA UTALII.

 



Na Mwandishi wetu, MVOMERO

WATUMISHI wa kada mbalimbali wa Wilaya ya Mvomero wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Saidi Nguya wameunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii  nchini kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Akizungumza na Waandishi wa habari juzi Wilayani humo  Saidi Nguya alisema Rais Dkt. Samia tangu aingie madarakani amekuwa mtu wa kwanza kuhakikisha kuwa Sekta ya utalii inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa.

Aliongeza kusema, hatua hiyo imeweza kuleta program ya Royal Tour kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.''Rais Samia amefanya kwa nafasi yake hivyo, watumishi wa Wilaya hiyo nao wanawajibu wa kuhamasishana ili kuonesha mchango wao katika kutangaza na kuhamasisha utalii,''amesema na kuongeza

''Sisi kwa nafasi yetu hapa kwenye ngazi ya Wilaya, Kata, Tarafa na ngazi ya Vijiji tunawajibu wa kuhamasishana sisi kwa sisi tuoneshe mchango wetu katika kuendeleza utalii wa ndani kwa kuhamasisha watu kutembelea mbuga zetu za wanyama,''amesema Said.

Sambamba na hilo,Saidi amebainisha kuwa moja ya majukumu yao kama wasaidizi wa Rais ni kutafsiri maono ya Rais Samia kulingana na mazingira waliyopo.

Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo amesema kuwa lengo mojawapo la ziara hiyo ni kuwapa nafasi wahudumu, waandishi waendesha ofisi na watunza kumbukumbu kutoka Taasisi mbalimbali za Wilaya hiyo ili wapumzike na kufurahia kutokana na kwamba kundi hilo limekuwa halitazamwi vizuri.

Saidi ameongeza kuwa, ubora wa ofisi unaanzia kwa kundi hilo kwa sababu ni kundi linalopokea wateja wengi, hivyo kundi hilo linatakiwa kupewa kipaumbele ili kupunguza ama kuondoa kabisa malalamiko ya wateja kuhusu ofisi au Taasisi husika.



Naye Afisa Uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Mikumi,David Kadomo aliwapongeza watumishi hao kwa ziara yao kwani wanahamasisha utalii wa ndani na kutoa rai kwa Wilaya zingine kuiga mfano wa Mvomero. ''Sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 17 kwenye pato la taifa hivyo kuna umuhimu wa kutunza hifadhi,''amesema.

Sambamba na hilo alipongeza pia jitihada za Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi hali ambayo imechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii kufikia zaidi ya laki moja katika hifadhi ya Mikumi kwa mwaka huu.

Kwa upande wao Watumishi wa Wilaya ya Mvomero akiwemo,Issaya Ramson ambaye ni Mtunza Kumbukumbu alisifu juhudi za Rais Samia kwa kuhamasisha utalii hapa nchini huku akitoa wito kwa Wilaya zingine kutembelea hifadhi hiyo.

Pia, amebainisha kuwa hifadhi hiyo ina wanyama mbalimbali kama vile Tembo, Twiga, Swala, Pundamilia, nyoka na ndege mbalimbali.

Naye Raheli Mgoni ambaye ni Mwandishi Mwendesha Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amesema jambo la watumishi hususani wa kada za waandishi waendesha ofisi, wahudumu na watunza kumbukumbu kutembelea hifadhi ya Mikumi halijawahi kufanyika, hivyo siku hiyo wamepata nafasi ya kubadilishana uzoefu na watumishi wengine lakini pia kujifunza masuala ya kitalii.


Powered by Blogger.