SAMIA ZIARANI CHINA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu  Hassan anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China Africa Cooperation - FOCAC) utakaofanyika kuanzia Septemba 4 - 6, 2024 jijini Beijing, China.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dares Salaam jana Agosti 31, 2024.

Waziri Kombo amesema Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki mkutano huo kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping.

Jukwaa la FOCAC lilianzishwa mwaka 2000 na Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika. Tangu kuanzishwa kwake jumla ya mikutano minane ikishirikisha wakuu wa nchi na serikali imefanyika.

Mikutano hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubadilishana kati va China na nchi moja wapo ya Afrika. Mkutano huu wa tisa wa FOCAC utafungulia na Rais Xi Jinping ambapo hotuba yake ya ufunguzi itatoa mwelekeo wa China katika uhusiano wake na nchi za Afrika.

Waziri Kombo amesema, tayari Serikali ya China imemteua Rais Samia Suluhu Hassan kuhutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano huo wa FOCAC akiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki.



Powered by Blogger.