TAHADHARI KWA UMMA
Anaandika Balozi wa Tanzania nchini Uingereza,Mbelwa Kairuki
"Uingereza ni moja ya sehemu ambazo wafanyabiashara wa Usafirishaji wa mizigo (transpoters) hununua maroli (used trucks) kwa ajili ya kupeleka Tanzania. Wanunuzi wengi hupendelea kununua maroli kutoka Uingereza kwasababu hapa Uingereza kama ilivyo Tanzania upande wa mwendeshaji upo kulia (Right hand driver); vilevile gharama ya used trucks ni nafuu; na pia imani iliyojengeka juu ya uimara wa magari hayo".
"Katika siku za karibuni Ubalozi umekuwa ukipokea malalamiko ya wafanyabiashara ambao wametuma pesa zao nchini Uingereza kwa ajili ya kununua maroli - lakini hawajatumiwa magari yao kwa muda unaozidi miezi 6 na wengine waliotumiwa wamepokea maroli yaliyo chini ya kiwango kwa mujibu ww makubaliano. Hali hiyo imepelekea usumbufu mkubwa na hasara kwa wafanyabiashara waliotuma pesa zao. Wengi wamechukua mikopo ya Benki na wanajikuta wanatakiwa kulipa madeni wakati magari yao hayajafika nyumbani kwa ajili ya kuanza shughuli za uzalishaji.
Kwa muktadha huo- Ubalozi unatoa tahadhari kwa wafanyabiashara wenye nia ya kununua maroli yaliyotumika kutoka Uingereza wachukue tahadhari za msingi wanapofanya manunuzi ili kuepuka usumbufu na hasara inayoweza kutokea.
Tahadhali za kuchukua ni pamoja na:
1) Kuhakikisha Kampuni unayotaka kufanya nayo biashara imesajiliwa nchini Uingereza (ipo active). Uhakiki huo unaweza kufanywa kupitia tovuti ya serikali ya Uingereza na hakuna malipo yoyote katika kufanya uhakiki: gov.uk/get-informatio…
2) Kuingia mkataba wa manunuzi na kampuni inayokuuzia roli. Wapo watanzania wanadiaspora wenye Ofisi za sheria (law firms) hapa nchini Uingereza ambao wanaweza kutoa huduma ya kuandaa mkataba na hata pale inapojitokeza changamoto zozote kuwa wepesi kwa wao kufuatilia kwasababu wapo on the ground.
3) Kufanya malipo kwa kutumia Letter of credit (LoC) badala ya kutuma pesa taslim moja kwa moja kwa kampuni kwa njia ya Telegraphic Transfer (TT). Utaratibu huu unafaa zaidi - kiasi cha malipo kinapokuwa ni kikubwa. Utaratibu wa Malipo kwa LoC unasaidia kukulinda pale muuzaji anapokiuka makubaliano - fedha hatolipwa na benki.
4) Kufanya upekuzi wa kufahamu historia ya roli unalotaka kununua kabla ya kufanya malipo. Ili kufanikisha upekuzi- ni vizuri upate Registration Number ya Gari iliyokuwa imesajiliwa nayo hapa Uingereza- kisha nenda katika tovuti ya Serikali ya Uingereza ambapo ina mfumo wa kutoa taarifa ya historia nzima ya gari- kama liliwahi kupata ajali, limefanyiwa check mara ngapi nk. Tovuti hiyo ni: gov.uk/check-mot-hist…
5) Kufanya ukaguzi kabla ya gari kusafirishwa (pre-shipment inspection) ili kujihakikishia kwamba kinachotumwa kinaendana na makubaliano yenu na mnunuzi."
Ubalozi unaamini njia tano zilizotajwa hapo juu zitawasaidia wenye nia ya kununua maroli kuepuka changamoto za manunuzi na usumbufu unaofuatilia katika kufuatilia kutokea mbali.