TCD, MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA SERIKALI WAKUTANA

 


Na Mwandishi wetu,DAR ES SALAAM

Viongozi Wakuu wa Vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) leo tarehe 18 Agosti 2024 wamekutana na kufanya mazungumzo na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mawaziri wa Wizara mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na TCD kupitia mitandao yake ya kijamii inaonesha kuwa kuwa kikao hicho kilichoongozwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kilijikita katika kujadili hali ya kisiasa nchini kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa hasa kutokana na sintofahamu ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na shughuli halali za vyama vya siasa vya upinzani.

Baadhi ya viongozi wakuu wa vyama hivyo walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Chadema, ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCD kwa sasa, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ndugu Dorothy Semu, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Ndugu Joseph Selasini, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR - Mageuzi. 


Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makatibu Wakuu John Mnyika (Chadema), Ado Shaibu (ACT Wazalendo), Hamad Masoud (CUF) na Faustine Sungura (Naibu Katibu Mkuu, NCCR Mageuzi).

Upande wa Serikali, uliwakilishwa na  Jenista Mhagama, Waziri wa Afya,Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria,  Dkt. Festo Ndugange, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na  Daniel Sillo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kikao hicho kimefanyika leo Jumapili, Agosti 18, 2024, jijini Dar Es Salaam.

Powered by Blogger.