BREAKING: KIONGOZI WA CHADEMA AKUTWA AMEUAWA
Mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)Taifa na Msaidizi wa Katibu Mkuu umekutwa Hospitali ya Mkoa wa Kinondoni, Mwananyamala katika chumba cha kuhifadhia maiti ukiwa umeharibika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Sept 8 2024 kupitia ukurasa wa mtandao wa X(zamani Twitter) na Mwanachama wa Chadema Boniface Jacob amesema, “mwili wa Ali Mohammed Kibao ulikutwa umetupwa jana alfajiri maeneo ya UNUNIO (jirani na viwanja vya NSSF) ukiwa na majereha makubwa sehemu za usoni kiasi ndugu zake walipata tabu kuutambua kirahisi”
Pichani: Mwenyekiti wa CHADEMA,Freeman Mbowe akiwa Hospitali ya Mwananyala uliko mwili wa Marehemu.Jacob ameeleza kuwa “kwa mujibu wa wenyeji wa Ununio ambao ni walima mchicha,wanasema Jana asubuhi walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi baada ya kuona mwili wa mtu mzima, mweupe mwenye asili ya kiarabu ambaye baadae Jana jioni ndugu waliutambua kuwa ni mwili Ali Mohammed Kibao ukiwa na majeraha”
Jeshi la Polisi halijatoa taarifa kuhusiana na tukio hilo, ingawa jana Jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake David Misime, jlilitoa taarifa ya kuanza uchunguzi wa kupotea kwa Kiongozi huyo.
ACT YALAANI
Chama cha ACT Wazalendo kimelaani vikali vitendo vya utekaji, mauaji, na kuumizwa kwa wanasiasa na wananchi kwa ujumla na maalumu kabisa ikilaani kuuawa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Ally Kibao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika makao makuu ya chama hicho, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Shangwe Ayo, amesema kuwa Watanzania wana haki ya msingi ya kuzungumza na kutoa maoni yao kwa uhuru.