ELIMU YA LAZIMA MIAKA 10 KUANZA 2027/28

 


Na Mwandishi Wetu, Ruvuma SERIKALI imesema utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 juu elimu ya lazima kuwa ya miaka 10 utaanza Mwaka 2027/28 ambapo wahitimu wa elimu ya msingi ya miaka 6 watakutana na wahitimu wa mwisho wa elimu ya msingi ya miaka saba na wataanza kidato cha  kwanza kwa pamoja.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Adolf Mkenda Mkoani Ruvuma jana  wakati akiwasilisha mada juu ya Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo 2023 kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Umoj wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi, Wenyeviti na Makatibu wa Wilaya  (UWT) ambapo alisisitiza kuwa ifikapo Mwaka 2027/28 Mtoto ambaye hatakaa shuleni kwa miaka 10 hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mzazi au mlezi.


Profesa Mkenda ameongeza kuwa ili kuhakikisha utekelezaji wa sera mpya unakwenda sawa bila kikwazo chochote, Serikali inaendelea na kufanya mapitio ya Sharia ya Elimu, Sura ya 353 ili iendane na mabadiliko yaliyomo katika Sera ya Elimu na Mafunzo mpya na kwamba mapitio hayo yatakapokamilika sharia hiyo itapelekwa bungeni 

“Tumeaua mtoto akae shuleni miaka 10, anaanza shule akiwa na miaka sita akifika darasa la saba anakuwa na miaka 13 tunasema elimu ya lazima imekwisha tunampa mtoto wa miaka 13 hiari ya kuamua kusoma au kutokusoma, je amefikia umri wa kufanya maamuzi hayo? Lakini akikaa kwa miaka 10 atatoka akiwa na miaka 16” amesema waziri huyo.

Aidha, Profesa Mkenda amengeza kuwa utekelezaji wa mitaala mipya unakwenda kwa awamu ili isiwe vurugu ambapo imeanza kutekelezwa kuanzia elimu ya Awali, darasa la kwanza na wanafunzi waliopo darasa la Mwaka 202 ambao watamaliza darasa la sita Mwaka 2027 na watalazimika kuendelea na kidato cha kwanza mpaka nne kwa lazima na kwa upande wa Sekondari walioanza na mitaala mipya ni wa mkondo wa Amali.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Caroylne Nombo amesema kuwa Wanafunzi wanaosoma Mkondo wa Amali watalazimika kusoma masoma matano ya lazima pamoja na moja la fani atakayochagua kutoka katika fani kuu 15 za katika mkondo huo.

Profesa Nombo ameyataja masomo hayo kuwa ni pamoja na Hesabu, Kiingereza cha Mawasiliano, Elimu ya Biashara ambalo ni lazima kwa wanafunzi wote Hisitoria ya Tanzania na Maadili ambalo litafundishwa kwa Kiswahili na atapaswa kuchagua lugha ya pili atakayoichagua.


“Shule 28 za serikali zimeanza kutoa mafunzo ya elimu ya amali na tunateg iliemea kuongeza shule za amali mbalimbali ili vijana wetu waweze kuingia katika kada mbalimbali za amali watakapomaliza masomo yao waweze kujiajiri ama kuajiriwa na wanaweza pia kuendelea na Diploma na kwenda kusoma Shahada ya fani aliyochagua” ameongeza Profesa Nombo.

Naye Mjumbe wa Mkutano huo Hawa Ghasia amesema kuwa mageuzi hayo ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 inaleta matumaini makubwa kwani unaiona nchi katika miaka 10 ijayo vijana watakuwa katika mazingira mazuri ambapo watatoka katika ngazi mbalimbali za elimu wakiwa na ujuzi utakaowawezesha   badala ya kusubiri kuajiriwa.

Powered by Blogger.