MBOWE AMDAI MSIGWA FIDIA YA 5B

 


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amempa siku tano aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyassa, Mchungaji Peter Msigwa, kuomba radhi na kulipa fidia ya shilingi bilioni 5 kutokana na madai ya kumkashifu na kuharibu chapa yake kutokana na matamshi ya Msigwa yaliyotolewa hadharani baada ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Katika barua (notisi ya madai) iliyotolewa Septemba 2, 2024 ikiwa na sahihi ya tarehe 4 Septemba, 2024, mawakili wa Mbowe ambao ni Hekima Mwasipu na wenzake kutoka Matwiga Law Chambers, Msigwa anadaiwa kutoa matamshi ya uongo na kumchafua Mbowe mbele ya umma.

“Msigwa alitumia majukwaa ya mikutano, vyombo vya habari, na hata mitandao ya kijamii kutoa madai ya kumkashifu mteja wetu,” ameleza Wakili Mwasipu.

Imeelezwa kuwa Msigwa alidai kuwa Mbowe ameanzisha "Mbowe Foundation," na anatumia chama cha CHADEMA kwa manufaa yake binafsi. Katika moja ya mikutano yake, Msigwa alinukuliwa akisema, "Mwenyekiti wa CHADEMA amegeuza chama kuwa SACCOS, fedha za chama zinaishia kwenye taasisi binafsi na si kwenye akaunti za chama.”

Mawakili wa Mbowe wameeleza kuwa matamshi hayo yameathiri sifa ya Mbowe ndani na nje ya Tanzania, hasa kutokana na nafasi zake mbalimbali kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia vya Afrika (DUA).

“Mteja wetu anaona maneno yote yanayozungumzwa na kunukuliwa hapo juu katika maana yake ya asili, muktadha na misemo kuwa ni kashfa, dharau na kudhuru sio tu sifa yake binafsi bali pia kwa familia yake yote, marafiki, taaluma (Siasa), Jumuiya ya Biashara, Jumuiya ya Kidini, marafiki na rika. Maneno haya si chochote lakini ushahidi dhahiri wa nia mbaya dhidi ya mteja wetu”, imeelezwa na mawakili.

Mbali na hilo, Msigwa alidai kuwa CHADEMA Digital ambayo ni huduma ya usajili wa wanachama, inamilikiwa na kampuni binafsi na kwamba Mbowe anatumia fedha za chama kwa manufaa binafsi.

“Hali hii imeleta hasara kubwa kwa mteja wetu kwani sifa yake ya kiongozi wa kisiasa, mfanyabiashara na mwanafamilia imeathirika sana,” alisema Mwasipu.

Kwa mujibu wa notisi hiyo, Msigwa anatakiwa kuomba radhi kupitia machapisho katika magazeti mawili; moja lenye kuweza kufikia nchi nzima na lingine ambalo linaweza kuwafikia watu walau wa kanda, na kulipa fidia ya Shilingi bilioni 5, la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa




 






Powered by Blogger.