TAASISI ZAIDI YA 40 ZAJITOKEZA KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA.



Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Angelista Kihaga amesema tangu kutangazwa kwa nafasi za kutoa elimu ya Mpiga kura kwa Umma zaiidi ya taasisi Arobaini zimejitokeza zikihitaji kupewa dhamana ya kutoa Elimu hiyo kwa Umma katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Bi. Angelista Kihaga amesema hayo katika mahojiano mubashara yaliofanyika kupitia kituo cha Televisheni cha TBC kupitia taarifa ya habari.

Amesema kumekuwa na mwitikio mzuri na mkubwa tangu Waziri mwenye dhamana ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alipotoa tangazo la Uchaguzi na kuruhusu matukio mengine kuendelea ambapo amesema zoezi lililopo ni kupokea maombi ya taasisi mbalimbali ambazo zitajihusisha na kutoa Elimu ya mpiga Kura.

Amesema baada ya kupokea maombi hayo, zoezi litakalofuata ni kupokea maombi ya Taasisi ambazo zitapenda kufanya uangalizi wa ndani wa Uchaguzi huu na baadae yatafanyiwa Uchambuzi na kupewa Kibali kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi za Serikali za Mitaa.

Bi. Angelista ameongeza kuwa Taasisi yeyote inayohitaji kuomba kutoa elimu ya Mpigakura mwisho ni Tarehe 06 September hivyo waendelee kuomba na zile Taasisi zinazotaka kuangalia Uchaguzi wa ndani ni lazima ziwe na sifa zote ambazo zimeainishwa katika tangazo ambapo ametaja miongoni mwa hizo lazima iwe imesajiliwa na mamlaka inayohusika na Usajili huo na mwisho wa kuomba ni tarehe 17 September,2024.

Powered by Blogger.