GWSON YAWAKUMBUKA WATOTO WENYE VICHWA VIKUBWA,MGONGO WAZI MOI


Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM 

KIKUNDI cha Wanawake waishio Goba(GWSON)kimetoa msaada wa vifaa tiba kwa Watoto wenye Vichwa vikubwa na Mgongo wazi kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI).

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo,leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa GWSON Marietha Kaole alisema msaada huo ni nyenzo muhimu katika kusaidia kundi hilo la watoto katika hospitali hiyo.

Amesema ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuhakikisha wanalinda na kutunza maisha ya wagonjwa kwa kuhakikisha wanawajali na kuwashika mkono.

'' Tumeona kuna uhitaji mkubwa wa vifaa tiba kwa watoto hao wa vichwa vikubwa na mgongo wazi,hivyo tukaona ni vema kuja kutoa msaada huu katika kumbukizi ya Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere na kumbukizi ya kuanzishwa kwa umoja wetu ambapo umefikia miaka mitatu hadi sasa,''amesema na kuongeza 

''Hii sio mara ya kwanza katika kutoa msaada huu tayari tumetembelea hospitali ya Ocean Road,Tumetoa msaada wa huduma za matibabu kwa watu mbalimbali kupima bure magonjwa ya upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi ,Matiti pamoja na Tezi Dume kwa wakazi wa Goba,''amesema.



Amesema GWSON ni kikundi cha wanawake walioamua kushirikiana 
katika kusaidiana kiuchumi na kijamii na kugusa wahitaji wale wadogo zaidi waliosahaulika katika jamii.

''Katika kikundi chetu kinaongozwa na kauli mbiu ya Mwanamke Jitambue ambayo imebeba maono ya Mwalimu Nyerere ya Kupinga Vita Adui,Ujinga,Maradhi na Umaskini,''amesema.



Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kikundi hicho,Salma Magesa amesema mbali na vifaa tiba pia wametoa mahitaji mengine kwa watoto hao kama Maji,Nguo,Pampers na Taulo za kike.

Amesema bado uhitaji wa vifaa mbalimbali kwa watoto hao unahitajika hivyo jamii iendelee kujitoa na kuwakumbuka katika kuwasaidia ili waweze kufarijika.

''Tumeguswa na jamii hasa watoto hawa ambapo  tumejichangisha fedha  kidogo na kuamua kuwaletea Dawa,maji,Taulo za Kike,Pampares,Nguo na hii ndio dhamira ya kuanzishwa kwa Kikundi hichi ambapo tuliamua kuisaidia jamii iliyotuzunguka,''amesema

Naye Afisa Ustawi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI),Sophia Nassoni amewashukuru kikundi hicho kwa kutoa msaada huo kwa watoto hao hiyo inaonyesha ishara ya upendo mkubwa kwa watoto hao.

Amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa tiba hivyo ambapo kwa mwaka wanawafanyia upasuaji  watoto hao 600 hadi 900 huku kwa watoto 1000 wanaozaliwa,watoto wanne hadi sita  wanazaliwa na ulemavu huo.

Ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidie watu hao na kutowaacha watu hao kwani wanauhitaji vitu mbalimbali ikiwemo Vitimwendo,Dawa na mrija wa punguza maji kwenye kichwa.


Powered by Blogger.