TISEZA YAKUTANISHA WATOA HUDUMA KUIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI
Na Mwandishi wetu,DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imekutana na zaidi ya watoa huduma 100 wa sekta ya uwekezaji kwa lengo la kuwarasimisha na kuongeza ubora wa huduma wanazotoa kwa wawekezaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TISEZA, Gireald Teri, amesema kikao hicho kinalenga kujenga ushirikiano wa karibu utakaosaidia kuimarisha uwazi, ufanisi na weledi katika kuwahudumia wawekezaji wanaoanzisha miradi nchini.
“Wawekezaji wengi wakija kufanya biashara na wawekezaji nchini huwa wanatumia kada mbalimbali za watoa huduma hapa nchini kwa kutafuta wanasheria ambao wanawasaidia kusajili makampuni, kutafuta ardhi kwaajili ya kuweka viwanda vyao, kuweka hesabu sawasawa , ulipaji wa kodi n.k”
Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda taswira ya Tanzania kama nchi salama kwa uwekezaji kwa kuondoa vitendo vya udanganyifu na kuwabaini watoa huduma wasio waaminifu.
“Sisi kama TISEZA tunawaita kwaajili ya kuwarasimisha ili tuweze kuwa tunashirikiana nao kwa ukaribu zaidi lakini pia kuhakikisha kwamba tunaweza tukalinda weledi katika eneo la kuwahudumia wawekezaji na kuhakikisha kwamba huduma zinazoenda kwa wawekezaji zinaleta taswira njema kwa nchi yetu lakini pia kuwaondoka wale waliokuwa wanawasumbua na kuwatapeli”amesema Teri
Ameeleza kuwa watoa huduma hao watapatiwa vyeti na leseni za muda maalum ili kuhakikisha wanazingatia maadili na viwango vya taaluma katika kazi zao.
“Tunawafanyia semina, tunawapa vyeti na leseni za kuwatazama kwa kipindi cha mwaka mmoja na tunawafundisha namna ya kutoa huduma kwa wawekezaji ili kuepuka wawekezaji kutumia watu ambao ni matapeli mwisho wa siku wanachafua na kuharibu taswira ya Tanzania kama sehemu salama ya kufanya uwekezaji”
Kwa upande wake, mdau wa kongamano hilo, Mathias Mhina kutoka Ofisi ya Wanasheria ya FIN & LAW, amesema urasimishaji huo utaongeza imani kwa wawekezaji na kusaidia kuweka gharama za huduma katika ushindani wa wazi, hali itakayorahisisha maamuzi ya kuwekeza nchini.
Naye mwezeshaji wa TISEZA, William Karage, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia mitaji zaidi, hatua itakayochochea ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa taifa kupitia uwekezaji wenye tija.




