WAZIRI MAVUNDE AZINDUA KIWANDA CHA NISHATI SAFI TABORA

 


Na Mwandishi wetu,TABORA 

WAZIRI wa Nishati Anthony Mavunde amezindua kiwanda kipya cha kuzalisha nishati safi ya mkaa wa kupikia cha Rafiki Briquettes kilichojengwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) eneo la viwanda Mtaa wa Kiloleni Mjini Tabora.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kiwanda hicho Mjini hapa leoWaziri Mavunde amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni utekelezaji azma ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuleta teknolojia rafiki ya nishati isiyo athiri mazingira.

Amebainisha kuwa kiwanda hicho ni fursa muhimu sana kwa wakazi wa Mkoa huo kwa kuwa kitahamasisha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia isiyo na madhara kwa mtumiaji.

‘Nakupongeza Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro na timu yako kwa kusimamia vizuri majukumu ya taasisi hii na kufanikisha ujenzi wa Kiwanda hiki, haya ni mafanikio makubwa, hongereeni sana’, amesema.

Waziri Mavunde amedokeza kuwa Kiwanda hiki ambacho kimegharimu takribani shilingi bilioni 3, kina uwezo wa kuzalisha tani 20 za mkaa kwa saa 1, hivyo akawataka kukisimamia ipasavyo ili kuongeza uzalishaji zaidi wa nishati hiyo.

Chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais, STAMICO ina uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi, ongezeeni uzalishaji katika kiwanda hiki na pale Kiwira kwenye makaa ya mawe ili kuongeza mapato zaidi, hiki ni kipindi cha kustawi.

Ameitaka Bodi na Watalaamu wa Shirika hilo kufanya kazi kwa weledi na uzalendo wa hali ya juu ili waweze kushindana na Makampuni makubwa ya Barrick na Geita Gold Mine (GGM) ambayo yanafanya vizuri sana katika sekta ya madini.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Balozi Simon Sirro amemweleza Waziri kuwa Shirika sasa liko vizuri na limejipanga kufanya mambo makubwa zaidi ikiwemo kuongeza uzalishaji wa nishati mbadala ya kupikia.

Akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Paulo Chacha, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella ameeleza kuwa wamepokea kiwanda hicho kwa mikono miwili kwa kuwa kitasaidia sana kuokoa mazingira.

Ameongea kuwa mbali na kuzalisha nishati safi ya mkaa pia STAMICO itawezesha wakazi 200 kupata ajira za uhakika kupitia Kiwanda hicho hali itakayochochea uchumi wa wananchi na Mkoa mzima.

Akitoa salamu za chama, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa Lucas Selelii aliyemwakilishi pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa, ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa serikali kupitia STAMICO kujenga Kiwanda hicho Mkoani hapa.

Amedokeza kuwa ujenzi wa kiwanda hiki ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana.







Powered by Blogger.