WAZIRI GWAJIMA AWATAKA WANAWAKE TANESCO KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Na Mwandishi wetu-Dar es salaam
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amewataka wanawake wanaofanya kazi katika Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), kuwa vinara wa mabadiliko katika kufanikisha ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika kongamano la pili la wanawake la nishati safi ya kupikia ya umeme, lililoandaliwa na wanawake wa TANESCO, Waziri Gwajima amesisitiza kuwa wanawake hao wanayo nafasi ya kipekee ya kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia umeme kama nishati safi, salama na nafuu.
Ameeleza kuwa takwimu zinaonesha asilimia 81 ya kaya nchini bado zinatumia nishati isiyo safi ya kupikia, hali inayowaathiri zaidi wanawake kiafya, kiuchumi na kijamii.
Amebainisha kuwa wanawake ndio wahanga wakuu wa madhara ya moshi wa kuni na mkaa, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na kupoteza muda mwingi kutafuta nishati hiyo hivyo aliwataka wanawake wa TANESCO kuanzia majumbani mwao kwa kutumia majiko ya umeme ili wawe mfano halisi kwa jamii.
Dk. Gwajima amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 hivyo lengo hilo haliwezi kufikiwa bila ushiriki wa sekta zote.
Ameitaja TANESCO kuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha umeme unatumika kikamilifu kuboresha maisha ya wananchi, hususan wanawake.
Aidha, amewahimiza wanawake wa shirika hilo kuwa mabalozi wa mabadiliko katika ngazi ya familia na jamii kwa kuondoa dhana potofu kuwa umeme ni ghali kwa matumizi ya kupikia na kueleza kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta majiko yanayotumia umeme kidogo na yenye gharama nafuu, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kung’ang’ania nishati zinazoharibu afya na mazingira.
Ametoa wito kwa wanawake wa TANESCO kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii na wadau wengine kueneza elimu kuhusu faida za nishati safi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema nafasi ya wanawake ndani ya shirika hilo inaheshimika na kuthaminiwa katika ngazi zote za uongozi hivyo aliwataka kuwa makini na kuendelea kudumisha mshikamano.
Ameongeza kuwa uongozi wa TANESCO unatambua mchango wa wanawake katika safari ya kulifikisha shirika mbele zaidi, akibainisha kuwa hakuna wakati ambao suala la kupandishwa vyeo au fursa mbalimbali limekuwa likipuuzwa bila kuzingatia usawa wa kijinsia.
Akiwahakikishia wafanyakazi wanawake kuwa sauti zao zinasikika na kuwa uongozi utaendelea kusimamia haki na maslahi yao kwa kuzingatia misingi ya usawa na haki kazini.
Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Twange ameeleza kuwa TANESCO linaungana na wanawake wengine duniani kuhimiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana sambamba na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2050.
Aidha, amegusia ajenda ya nishati safi ya kupikia, akisema shirika linaunga mkono juhudi za serikali zinazoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Amebainisha kuwa TANESCO ina mpango wa kusambaza majiko ya umeme kwa watumishi wake na kuendelea kuhamasisha wananchi kuachana na nishati zisizo salama.
Hatahivyo Twange alisisitiza kuwa shirika litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo wizara husika, kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa kwa vitendo.








