MAKONDA ASIMAMISHA UCHAGUZI.KAMATI YA OLIMPIKI TANZANIA TOC
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesimamisha uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) pamoja na uongozi wa sasa wa kamati hiyo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kushiriki katika uchaguzi uliokuwa ufanyike Aprili 12, 2026.
Wagombea hao wamelalamikia mchakato huo kukosa uwazi, uwajibikaji na haki, wakidai vyombo vilivyosimamia uchaguzi havikutenda kwa usawa, jambo lililosababisha sintofahamu na taharuki miongoni mwa wadau wa michezo.
Aidha, Waziri Makonda amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuheshimu misingi ya kimataifa ya uhuru wa vyama vya michezo kama inavyoelekezwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), lakini uhuru huo hauondoi wajibu wa kuhakikisha taasisi zinaendeshwa kwa kuzingatia utawala wa sheria, haki, uwazi na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.
Amesema amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka ya kisheria aliyonayo katika kusimamia sekta ya michezo, ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa, Sura ya 49, zinazompa jukumu la kuhakikisha taasisi zote zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria na kanuni.
Makonda ameongeza kuwa amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mchakato wa uchaguzi ulikiuka misingi ya utawala bora na kuonekana kuwanufaisha watu wachache, hali inayoweza kudhoofisha maendeleo ya michezo nchini.

