VIJANA WATAKIWA KUENDELEZA ALAMA ZA WAASISI WA MUUNGANO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amewataka vijana na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu nchini kuendeleza na kulinda misingi ya Muungano iliyoasisiwa na viongozi waasisi wa Tanzania, akiwemo Abeid Amani Karume na Julius Kambarage Nyerere.
Mhe. Masauni ametoa wito huo Aprili 6, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano maalum la kumuenzi Abeid Amani Karume, kuelekea maadhimisho ya Karume Day.
Amesema kiongozi huyo ameacha historia na alama ya kudumu kutokana na mchango wake mkubwa katika kuunganisha Watanzania na kupigania maslahi ya wananchi, hususan katika nyanja za kiuchumi, pamoja na kupinga ukabila na ubaguzi.
“Leo tunapomuenzi Sheikh Abeid Amani Karume, tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake, hususan juhudi zake za kuasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964,” amesema Mhe. Masauni.
Ameongeza kuwa kiongozi huyo alikuwa imara katika kusimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar, na kwamba juhudi hizo zimeendelea kuenziwa na serikali katika awamu mbalimbali za uongozi.
Aidha, ameeleza kuwa Abeid Amani Karume atakumbukwa kwa sera zake zilizogusa maisha ya wananchi wengi, zikiwemo ugawaji wa ardhi bure, elimu bila malipo, huduma za afya bure na ujenzi wa makazi ya kisasa.
“Aliishi ndoto ya umoja wa Afrika kwa vitendo, akihamasisha kuunganishwa kwa Bara la Afrika kupitia dhana ya shirikisho,” alisisitiza Masauni.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema kongamano hilo ni la kwanza kufanyika Tanzania Bara na lina lengo la kuwahamasisha vijana kutambua mchango wa waasisi wa Muungano.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa programu maalum ya elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu Muungano, ikiwalenga makundi mbalimbali yakiwemo vijana na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Kongamano hilo la siku moja limeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Kwa upande wao washiriki wa kongamano hilo wamesisitiza umuhimu wa vijana kuendeleza tunu za Muungano na uzalendo.
Mhandisi Matiko Matiasi amesema kuwa hayati Karume ameacha dira ya maendeleo ambayo vijana wanapaswa kuifuata kwa vitendo, huku wakilinda amani na mshikamano wa taifa.
Naye Tunu Kalanje amebainisha kuwa kila kijana anapaswa kuwa mzalendo kwa kuitanguliza nchi mbele, kama ilivyokuwa kwa muasisi huyo.


.jpg)