RAIS DKT.MWINYI: SERIKALI KUUNDA KAMATI MAALUM KUFUATILIA MAPENDEKEZO YA RIPOTI YA FIDIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaunda Kamati Maalum ya Uratibu kwa kipindi cha miezi mitatu kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Tathmini ya Masuala ya Fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo.
Akizungumza leo tarehe 12 Mei 2026 Ikulu Zanzibar baada ya kupokea ripoti ya Tume hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuhusika na udanganyifu, upotevu wa fedha za fidia na matumizi mabaya ya fedha za umma, huku akisisitiza kuwa fedha zote zilizopotea lazima zirejeshwe Serikalini.
Aidha, ameiagiza ZAECA kuchunguza upotevu wa fedha na kumbukumbu za malipo ya fidia pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika. Serikali pia imepokea pendekezo la kuanzishwa kwa Mfuko Maalum wa Fidia kwa lengo la kuongeza uwazi na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali.
Rais Dkt. Mwinyi amepongeza kazi iliyofanywa na Tume hiyo na kueleza kuwa ripoti hiyo ni miongoni mwa ripoti bora zilizowahi kuwasilishwa Serikalini.

