MKUU MKOA WA DAR ES SALAAM,ALBERT CHALAMILA AWAHAKIKISHIA USALAMA WAKUTOSHA WANANCHI NA WAGENI WAKATI WA MAONESHO YA SABASABA.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewahakikishia wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya nchi usalama wa kutosha wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Akizungumza Dar es Salaam leo, Chalamila amesema maandalizi yote ya usalama yamekamilika kabla ya ufunguzi wa awali utakaofanyika Juni 28 na ufunguzi rasmi Julai 3, 2026.
Chalamila amesema maonesho hayo yatashirikisha mataifa mbalimbali yakiwemo China, Misri, Rwanda, Japan, Poland, Korea Kusini, Falme za Kiarabu, Singapore, Kenya, Uganda na mengine mengi, jambo linaloonyesha hadhi ya kimataifa ya Sabasaba.
Aidha, ameeleza kuwa maonesho hayo yataendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa kuongeza fursa za biashara, uwekezaji na upanuzi wa masoko kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali imeboresha huduma za usafiri kuelekea viwanja vya maonesho, ikiwemo usafiri wa mwendokasi, huku pia ikihakikisha huduma za afya na taratibu za kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko zinapatikana kwa washiriki wote.


