SERIKALI YAONGEZA AJIRA KWA VIJANA NA WANAWAKE KUPITIA SEKTA YA UTALII

 



BUNGENI DODOMA, JUNI 26,2026


NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia Sekta ya Utalii nchini ili kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.



Mhe. Chande amesema hayo leo Juni 26, 2026, katika Bunge la 13, Mkutano wa Tatu, Kikao cha 58, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi, aliyetaka kufahamu mkakati serikali katika kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia Sekta ya Utalii.


“Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha mafunzo ya ujuzi wa kazi za utalii na ukarimu kupitia vyuo vya utalii, kuongeza fursa za uwekezaji katika huduma za utalii, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa vijana na wanawake katika biashara na shughuli za usafirishaji watalii, uongozaji watalii, miradi ya utalii wa kiutamaduni na malikale na huduma za malaz,i” alifafanua Mhe. Chande.


Mhe. Chancde ameongeza kuwa katika kufikia malengo hayo, Wizara imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika Sekta ya Utalii ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuongeza fursa za ajira ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho ya kanuni za usajili na utoaji leseni, kupunguza ada ya leseni  kutoka Dola za Marekani 2000 hadi Dola za Marekani 500.


Ametaja hatua nyingine iliyochukuliwa kuwa ni kupunguza gharama za malipo ya leseni za waongoza watalii kutoka Dola za Marekani 50 hadi Shilingi 35,000 kwa mwaka sambamba na kutoa mafunzo kwa waongoza utalii zaidi ya 2,200 nchini ambapo mikakati hiyo imewezesha Watanzania wengi wakiwemo vijana na wanawake kuingia katika biashara ya utalii na kupata fursa ya ajira za kuongoza watalii.

Powered by Blogger.