TUME YA MADINI YAACHA ALAMA MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA
Wananchi Wapata Elimu Kuhusu Leseni, Uchimbaji na Fursa za Sekta ya Madini
Wakati Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yakifikia tamati leo katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma na kufungwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe Tume ya Madini imehitimisha ushiriki wake kwa mafanikio makubwa baada ya kuwafikia mamia ya wananchi waliotembelea banda lake kwa ajili ya kupata elimu kuhusu sekta ya madini.
Katika kipindi chote cha maonesho hayo, wataalam wa Tume ya Madini kutoka kurugenzi mbalimbali walitoa elimu kuhusu taratibu za upatikanaji wa leseni za madini, usimamizi wa shughuli za uchimbaji, biashara ya madini, ukaguzi wa migodi pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.
Banda la Tume ya Madini lilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyovutia idadi kubwa ya wageni waliotaka kufahamu kwa undani mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa, sambamba na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha rasilimali za madini zinachimbwa, zinachakatwa na kuuzwa kwa kuzingatia sheria, usalama, afya na uhifadhi wa mazingira.
Wananchi waliotembelea banda hilo walieleza kuridhishwa na elimu waliyoipata, wakibainisha kuwa imewawezesha kuelewa kwa kina zaidi majukumu ya Tume ya Madini na namna wanavyoweza kushiriki katika shughuli za sekta hiyo kupitia umiliki wa leseni halali pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na utoaji wa huduma zinazozunguka sekta ya madini.
Ushiriki wa Tume ya Madini katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma umeendelea kudhihirisha dhamira ya taasisi ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma na kuhamasisha ushiriki mpana wa Watanzania katika maendeleo endelevu ya sekta ya madini nchini.



