AAT NA POLISI WAANZISHA MAPAMBANO DHIDI YA AJALI ZA BARABARANI KUPITIA ELIMU KWA WATOTO WA SHULE
Na Mwandishi Wetu--Dar es salaam
Chama cha Mbio za Magari Tanzania (AAT), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, kimeendelea kutekeleza mradi wa FIA Safe and Sustainable Mobility Grant Programme unaolenga kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wenye umri chini ya miaka 18 katika shule 19 za msingi na sekondari zilizopo Wilaya ya Ubungo, ili kupunguza ajali zinazowakumba watoto.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu, Joseph Mwakabonga, alisema watoto ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata ajali kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri na msongamano wa magari, hasa katika maeneo ya shule.
Alisema ajali za barabarani zinaendelea kusababisha vifo, majeruhi na ulemavu wa kudumu, huku watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, waendesha pikipiki na watoto wakiwa makundi yanayoathirika zaidi.
Mwakabonga alisisitiza kuwa suluhisho la changamoto hiyo ni kuanza kuwajengea watoto uelewa wa usalama barabarani tangu wakiwa shuleni ili wajifunze matumizi sahihi ya barabara na kuheshimu sheria za usalama.
"Usalama barabarani si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuanzia Serikali, taasisi, shule, wazazi hadi wananchi kwa ujumla," alisema.
Aidha, aliwataka madereva wa vyombo vyote vya usafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani, akibainisha kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa jamii
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Utawala wa AAT, Hanif Virji, alisema kupitia mradi huo, AAT imetekeleza maboresho mbalimbali katika shule 19 za Wilaya ya Ubungo ikiwemo kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu pamoja na kuboresha miundombinu ya usalama kwa kuweka alama za barabarani, michoro ya usalama, vivuko vya waenda kwa miguu (zebra crossing) na matuta ya kupunguza mwendo wa magari.
Alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapoingia na kutoka shuleni, sambamba na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika familia na jamii zao.
Naye mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibasila, Leticia Pascal Martin, alisema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya barabara na utambuzi wa alama mbalimbali za usalama.
Alisema maarifa hayo yatawasaidia kujilinda wanapokuwa barabarani na pia kuwafundisha wazazi, ndugu na jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria za usalama barabarani
Pia aliwataka madereva kuzingatia alama za barabarani na kufuata sheria zote za usalama ili kupunguza ajali ambazo zinaweza kuzuilika.
Mradi wa FIA Safe and Sustainable Mobility Grant Programme unatarajiwa kuendelea kuongeza uelewa wa usalama barabarani kwa watoto na kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, AAT, shule na wadau mbalimbali katika juhudi za kupunguza ajali za barabarani nchini.




