RAIS SAMIA APELEKA TABASAMU KWA WANANCHI KALIUA
Na Mwandishi wetu,Kaliua
WAKAZI wa Kata zaUgunga, Ushokola na Ufukutwa Wilayani Kaliua Mkoani hapa wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Rais Dkt Samia Suluhu
Hassan kupeleka zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo kipya cha afya katika Kata ya Ugunga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa waliotembelea Wilaya hiyo jana wameishukuru serikali kwa kusikia kilio chao.
Mkazi wa Kijiji cha Ugunga Amina Chunga (65) ameeleza kuwa mradi huo umekuja wakati mwafaka kwa kuwa wananchi walikuwa wanapata shida sana kufuata huduma umbali mrefu.
Amefafanua kuwa usiku ilikuwa mtihani mgumu sana kwa wakazi wa Kata hiyo na maeneo jirani wanapopata changamoto za kiafya, kwani hulazimika kukodi bodaboda kwa gharama kubwa kwenda hospitali ya Wilaya.
Diwani wa Kata ya Ushokola ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Anastazia Bebete amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwapatia kiasi hicho ili kujenga Kituo hicho.
Amesisitiza kuwa Kituo hicho ambacho kitahudumia wakazi zaidi ya 20,000 wa Kata hiyo na Kata jirani za Ushokola na Ufukutwa kitasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto na jamii nzima.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo Enock Tama ameeleza bayana kuwa Rais Samia ameleta tabasamu kwa wananchi kwa kuwa mradi huo ilikuwa kilio chao cha muda mrefu.
‘Namshukuru sana Mhesh.Rais kwa kutuletea zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hiki ili kurahisisha upatikanaji huduma za afya kwa wakazi wa Kata hii na Kata jirani’, ameongeza.
Aidha amemshukuru kwa kuwapatia zaidi ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Lufungija sekondari ambayo tayari imekamilika na shule mpya ya msingi Ukombozi.
‘Shule hizi ni za viwango vya hali ya juu, zimejengwa kwa weledi mkubwa, watoto watakaosomea katika shule hizi hawana utofauti na mtoto anayesoma chuo kikuu’, ameleza.
Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Gerald Mongela ameeleza kuwa ubora wa miradi hiyo umechangiwa na usimamizi mzuri wa Wataalamu na Ofisi ya Mkurugenzi.
Akisalimia wananchi katika Wilaya hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Nkuba ameeleza kufurahishwa na usimamizi mzuri wa miradi yote iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya hiyo na Wilaya nyingine.
Ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya hiyo kutunza miundombinu ya miradi hiyo ili iendelee kutumika kwa manufaa ya familia zetu, vizazi vya sasa na vijavyo pia.



