UHAMIAJI: WAENDESHA VYOMBO VINAVYOVUKA MIPAKA WATAKIWA KUWAFIKISHA RAIA WA KIKEGENI WASIOJULIKANA KATIKA VITUO HUSIKA

 




Na Mwandishi wetu--Dar es salaam


Kamishna wa Uhamiaji wa Kitengo cha Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, CI Fakin Nyakunga, amewataka waendesha vyombo vya moto vinavyovuka mipaka ya nchi, ikiwemo pikipiki, bajaji, teksi, mabasi na malori, kuhakikisha wanawafikisha raia wa kigeni wasiojulikana katika vituo vinavyohusika kwa mujibu wa sheria badala ya kuwaacha kuendelea na safari bila utambuzi.



CI Nyakunga alitoa wito huo Julai 12, 2026, alipotembelea Banda la Idara ya Uhamiaji katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam. Alisema Idara hiyo inaendelea na kampeni ya "Mjue Jirani Yako", inayolenga kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, hususan waendesha vyombo vinavyovuka mipaka, kuhusu umuhimu wa kushirikiana na mamlaka za uhamiaji katika kudhibiti uhamiaji usio halali.




Alieleza kuwa ushirikiano wa madereva na waendesha vyombo vya usafiri utasaidia kupunguza idadi ya watu wanaoingia au kuishi nchini bila kuwa na vibali halali.


"Sheria ya Uhamiaji ipo na inafanya kazi. Hivyo, wewe unayetumia chombo cha moto na unavuka mipaka, unapokutana na raia wa kigeni usiyemtambua, ni vyema umfikishe katika kambi ya wakimbizi au kituo cha polisi kilicho karibu kwa ajili ya taratibu za kisheria," amesema CI Nyakunga.




Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi ili kuimarisha usalama wa mipaka na kuhakikisha sheria za uhamiaji zinafuatwa kwa manufaa ya taifa.

Powered by Blogger.