WAWEKEZAJI WA UCHINA WAONYESHA NIA KUJA KUWEKEZA VIWANDA VYA DAWA NCHINI
Na mwandishi wetu.
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amethibitisha dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba kupitia ushirikiano wa kimkakati na wawekezaji makini kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza leo alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Shandong Hongyu Medical Technology Group Co., Ltd mjini Weihai, nchini China, Mhe. Mchengerwa amesema kampuni hiyo ni miongoni mwa wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya dawa na vifaa tiba katika Eneo Maalum la Uwekezaji wa Viwanda vya Dawa la Mloganzila, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Bw. Miao Yingyang, Waziri amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza viwanda vya dawa, akisisitiza kuwa ushirikiano na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya.
Aidha, ameeleza kuwa Eneo Maalum la Kiuchumi la Mloganzila ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika kukuza uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba. Amesema eneo hilo linatarajiwa kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za afya kwa soko la ndani na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Waziri Mchengerwa amesema Wizara ya Afya itaendelea kuwa mshirika hai katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji badala ya kuwa mdhibiti pekee. Ameongeza kuwa mfumo wa uwekezaji nchini unaongozwa na sheria na taratibu zilizo wazi zinazolenga kuwapa wawekezaji mazingira bora ya kufanya biashara.
Amefafanua kuwa Serikali inalenga kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha dawa na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuimarisha usalama wa afya na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa wananchi wakati wote.
Aidha, amesema azma ya Tanzania ya kujitegemea katika sekta ya afya haimaanishi kujitenga na washirika wa maendeleo, bali kujenga ushirikiano wa muda mrefu unaozingatia manufaa ya pande zote, heshima na uwekezaji wenye tija kwa maendeleo ya sekta hiyo.



