BALOZI YAKUBU: MAZAO MAPYA YA UTALII YATAVUTIA ZAIDI YA WAGENI MILIONI 10 KUTOKA UFARANSA KUTEMBELEA TANZANIA.*

 






Na mwandishi wetu


Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Mhe. Saidi Othman Yakubu ameeleza kuwa mazao mapya ya utalii na utangazaji wa vivutio katika miji ya Ufaransa ndivyo vitakavyoibua wageni wengi kutembelea Hifadhi za Taifa Tanzania.


Aliyasema hayo leo Agosti 19, 2026 Mkoani Kilimanjaro alipotembelea Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na kufanya kikao na menejimenti ya Hifadhi juu ya maombi ya kibali cha mradi wa viberenge (Cable Car) kutoka UNESCO kuweza kutumika katika hifadhi kutoka lango la Machame hadi kituo cha Shira.


Akizungumza katika kikao hicho Balozi Yakubu alisema "Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro wanakusudia kuanzisha mradi wa viberenge mradi ambao umeombewa kibali UNESCO. Kwa hiyo kuna mambo ambayo tumeyaainisha, na namna bora ya kuyaendea sisi ambao tuko Paris kuhakikisha yanafanyiwa kazi ili kuongeza tija katika sekta ya utalii nchini".


Aliongeza kuwa kutokana na upekee wa Hifadhi, matangazo (Roadshow) katika miji kama vile Marseille, Paris, Lyon na Lille yataongeza tija ya kuwavutia wenyeji takribani Milioni 68, ambako Milioni 15 kati yao husafiri kutalii maeneo mbalimbali duniani kila mwaka.


Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Angela Nyaki, alieleza kuwa mradi huu wa viberenge utaongeza idadi kubwa ya watalii hususan utalii wa siku moja yaani (Day trip) pamoja na kurahisisha zoezi la uokoaji pindi dharura ya kiafya inapojitokeza mlimani. Kadhalika Hifadhi imeshafanya maandalizi ya awali ikiwemo kupata mwekezaji kutoka Avan Kilimanjaro Limited kutekeleza mradi huo.


Hatua hii inatajwa kuwa kichocheo muhimu katika kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii la kimataifa, huku mazao mapya ya utalii yakilenga kuvutia zaidi ya watalii kutoka Ufaransa na maeneo mengine duniani na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa.

Powered by Blogger.