BIL 31 KUKAMILISHA BARABARA YA LAMI KIBONDO MJINI

 




Na mwandishi wetu, Kibondo


SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka shilingi bil 31.9 kukamilisha matengenezo ya km 25.9 za barabara ya lami ambayo ni mchepuko wa barabara kuu inayoingia Kibondo Mjini.


Ujenzi wa barabara hii inayoanzia eneo la Nduta Junction kupitia vijiji vya Malolegwa, Kitahana na Twabagondozi hadi Kibondo Mjini ambayo awali iliishia kwenye makutano ya barabara ya Mabamba unatarajia kukamilika Desemba 2026.




Akizungumzia na gazeti hili hivi karibuni, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Edson Edward amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu sana kwa kuwa itarahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa na mazao ya wananchi.


Ametaja mazao makuu yanayolimwa katika Wilaya hiyo kuwa ni maharage, mahindi, parachichi na mihogo na kudokeza kuwa kukamilika kwake kutawezesha wakulima kufikisha mazao yao sokoni kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi.




‘Kukamilika kwa mradi huu unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 31.9 kutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa Wilaya hii na Mkoa mzima wa Kigoma ikiwemo Mikoa jirani’, ameongeza.


Mhandisi Edward ameeleza kuwa serikali pia imetoa shilingi milioni 350 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wakazi wa Wilaya hiyo walioathiriwa na mradi, hali ambayo imewezesha upatikanaji wa eneo la ujenzi na kuendelea kwa kazi bila vikwazo.


Wakiongea kwa nyakati tofauti wakazi wa Vijiji vya Malolegwa, Kitahana na Twabagondozi wamemshukuru sana Rais Samia kwa kutoa fedha za kukamilisha kipande hicho ambacho kimekuwa kero kubwa, sasa lami itafika Kibondo Mjini.


Joyce Wachu na Mohamed Lulaho wakazi wa Kitahana wameeleza bayana kuwa  barabara hiyo itawasaidia kukuza biashara zao, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuongeza thamani ya mazao yao kutokana na urahisi wa usafirishaji.


Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu inayotekelezwa katika Mkoa huo, ukiwa na lengo la kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wa Wilaya hiyo na maeneo jirani.



Powered by Blogger.