PAUL CHACHA: WASANII, WANAHABARI WANAFANYA KAZI NZURI






 Tabora

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kufurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na wasanii na wanahabari nchini kwa kuwa wanaburudisha na kuhabarisha umma juu ya matukio mbalimbali kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa NEC Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa Paul Matiko Chacha alipokuwa akihutubia umati wa wanaCCM, Viongozi na wakazi wa Mkoa wa Tabora waliojitokeza kumpokea jana Mjini hapa.

Chacha amepinga vikali kauli iliyotolewa hivi karibuni na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche akidai kuwa wanahabari wanaandika upumbavu na wasanii hawatendei haki wananchi.

Amesisitiza kuwa wasanii, wanahabari na timu za mpira ikiwemo Simba na Yanga wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa maslahi yao pia, hawafanyi upumbavu kama anavyodai Makamu Mwenyekiti Heche.

‘Wanahabari hawaandiki upumbavu, wanatekeleza majukumu yao tena kwa weledi mkubwa na wasanii hawafanyi mambo ya kipumbavu, wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, haya maneno ya ndugu yangu Heche hayafai hata kidogo’, ameeleza.



Chacha ameongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi kina mipango mizuri ndio maana kinashinda chaguzi, na kuongeza kuwa hata kauli ya baadhi ya wapinzani kuwa CCM inaiba kura haina maana yoyote kwa kuwa hakuna wa kuwapigia kura.

‘Chama ambacho hakina mipango endelevu hakiwezi kuongoza nchi, hata kikipewa madaraka wataishia kuvurugana tu, kwa sasa mbali na CCM hakuna chama chenye uwezo wa kuongoza nchi, vyama vyote bado vichanga’, ameeleza.

Amebainisha kuwa kauli zinazotolewa na Makamu Mwenyekiti Heche hazina hekima wala msingi wowote hivyo akamtaka kwenda kuwaomba radhi wazee, akiwemo Mzee Mbowe na familia ya Chacha Wangwe.

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Juma Nkumba ameeleza kuwa wanaCCM na wakazi wote wa Mkoa huo wamepokea uteuzi wake kwa furaha na majonzi kwa kuwa walimpenda sana na walitamani aendelee kuwa Mkuu wao wa Mkoa. 

Amebainisha kuwa mapokezi makubwa waliyompa ni ishara ya upendo wao wake na kuthamini kazi nzuri aliyofanya katika Mkoa huo na kuahidi kuwa wataendelea kumpa ushirikiano katika majukumu yake mapya ya Kitaifa.  

Powered by Blogger.