UVINZA, BUHIGWE WAIBUKA KIDEDEA MAONESHO YA NANE NANE TABORA
Na Mwandishi wetu, Tabora
HALMASHAURI za Wilaya ya Uvinza na Buhigwe za Mkoani Kigoma zimelipuka kwa shangwe na furaha baada ya kuibuka kidedea kwenye Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kanda ya Magharibi yaliyomalizika jana Mjini hapa.
Maonesho hayo yaliyosheheni bidhaa mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi zilizooneshwa na makampuni, taasisi na wadau mbalimbali, yalianza Agosti 1 na kuhitimishwa Agosti 8 katika Viwanja vya Nane Nane Ipuli, Mjini Tabora.
Halmashauri ya Uvinza imeibuka mshindi wa kwanza kwenye kundi la Mamlaka za Serikali za Mitaa ikifuatiwa na Halmashauri ya Buhigwe zote kutoka Mkoani Kigoma huku Halmashauri ya Igunga ya Mkoani Tabora ikishika nafasi ya tatu.
Na kwa ushindi wa jumla Jeshi la Magereza limeibuka mshindi wa kwanza likifuatiwa na Halmashauri ya Uvinza na Buhigwe hali iliyoibua shangwe kutoka kwa wawakilishi wa Wilaya hizo wakiwemo watumishi.
Jumla ya halmashauri 16 zilishiriki maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka katika Kanda hiyo ambapo 8 ni za Mkoa wa Tabora na 8 za Mkoa wa Kigoma, zikiwemo taasisi, mashirika, makampuni, na wadau wa kilimo.
Akiongea kwenye kilele cha maadhimisho hayo jana Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Dkt Rajabu Seif amepongeza halmashauri na taasisi zote zipatazo 200 zilizojitokeza kushiriki mwaka huu.
Amedokeza kuwa jumla ya taasisi 1,680 zilileta bidhaa zao katika maonesho hayo yanayodhaminiwa na Benki ya NMB hali iliyochochea hamasa na wananchi wengi zaidi kujitokeza ili kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo bora na teknolojia .
Amefafanua kuwa dhamira ya serikali ni kuona maonesho hayo yanaleta tija kwa wakulima, hivyo akaagiza Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha elimu inayotolewa katika maonesho hayo inahamishiwa kwa wakulima vijijini.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora IGP Mstaafu Simon Sirro ameeleza kuwa maonesho hayo ni muhimu sana kwa kuwa yanachochea ukuaji wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Amemhakikishia kuwa elimu ya kilimo bora na matumizi sahihi ya teknolojia sasa vitahamishiwa vijijini chini ya usimamizi wa Maafisa Kilimo na Mifugo ili kuhamasisha kilimo chenye tija na ufugaji bora kwa uchumi wa wananchi.





