WIZARA YA AFYA YAENDELEA KUIMARISHA UWEZO WA WATUMISHI WA AFYA KUKABILIANA NA DHARURA, UGONJWA WA EBOLA
Akizungumza leo Agosti 6, 2026, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Longido, Dkt. Matthew Adoniz, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha vituo vya kutolea huduma vinaendelea kuwa tayari kutoa huduma salama, zenye ubora na kwa wakati wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Amesema mafunzo hayo yameongeza uwezo wa watumishi wa afya kutumia miongozo ya kitaifa katika utoaji wa huduma za dharura, kuimarisha uratibu wa huduma kwa wagonjwa mahututi pamoja na kuongeza utayari wa kituo hicho kukabiliana na matukio ya dharura za afya ya umma.
Dkt. Adoniz amesema kuwa, kutokana na Kituo cha Afya Eworendeki kuwa karibu na mpaka wa kimataifa, kituo hicho kina nafasi muhimu katika kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko, ambapo kina uwezo wa kutambua wasafiri wanaoweza kuwa na dalili zinazohusiana na Ebola kupitia utaratibu wa uchunguzi wa afya (screening) kwa wasafiri wanaoingia nchini.
Aidha, amesema kituo hicho kina eneo maalumu la kutenga watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi (Isolation Room), lenye mazingira salama yanayowezesha utoaji wa huduma za awali wakati taratibu za kuwahamishia wahusika katika vituo maalumu vya matibabu zikiendelea.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Theresia Haule, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Afya za kuendelea kuimarisha utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kukabiliana na dharura za afya ya umma, ikiwemo milipuko ya magonjwa kama Ebola.
Amesema maandalizi yanayoendelea kufanyika katika vituo vya afya vilivyopo maeneo ya mipakani yanaonesha dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuimarisha mifumo ya ulinzi dhidi ya magonjwa ya mlipuko, hususan kutokana na uwepo wa changamoto za magonjwa ya kuambukiza katika baadhi ya nchi jirani.



