DKT PIMA AAHIDI NEEMA KWA WAFUGAJI

 




Na Mwandishi wetu, Tabora


MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt John Pima ameahidi kutoa mbegu bora za upandishaji mitamba ya ng’ombe kwa wafugaji waliopo katika kata zote za manispaa hiyo ili kuongeza uzalishaji wa mifugo bora.




Dkt Pima ameeleza hayo jana alipokuwa akitoa taarifa kwenye kikao cha madiwani, wataalamu, watendaji, viongozi wa chama na serikali, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na wanahabari.


Amesema kuwa kwa mwaka huu wameandaa mbegu 1000 za upandishaji mitamba ya ng’ombe (majike) ambazo zitagawiwa bure kwa wafugaji waliopo katika maeneo mbalimbali ndani ya manispaa hiyo ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji.



‘Mifugo ni chanzo kizuri cha mapato, hivyo tumedhamiria kuwa na ufugaji wa kisasa katika manispaa yetu na kwa kuanzia tutagawa bure mbegu ili kuchochea uzalishaji wa mifugo bora, hili litasaidia kuongeza idadi ya mifugo pia’, amedokeza.  


Dkt Pima amebainisha kuwa zoezi hili litakuwa endelevu katika manispaa hiyo ili kuleta mageuzi chanya kwenye sekta ya mifugo na ufugaji katika halmashauri hiyo na Mkoa mzima wa Tabora.


Katika kikao hicho ametambulishwa mmoja wa wafugaji wanaofanya vizuri ambaye mwaka huu ameshika nafasi ya pili Kitaifa kwa ufugaji bora na kutunukiwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan cheti na zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni 8.


Mfugaji huyo Paschal Said Bilolele mkazi wa Kata ya Ikomwa katika manispaa hiyo ameibuka mshindi wa pili Kitaifa kwenye Kundi la Wafugaji wa nchi nzima katika Maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika Kitaifa Jijini Dodoma mwaka huu.


Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ghullam-Hussein Dewj amemkabidhi zawadi ya cheti cha pongezi na kitita cha shilingi laki 5 zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa hiyo kama ishara ya kutambua kazi yake njema kwenye sekta hiyo.


Amepongeza Ofisi ya Mkurugenzi kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa tuzo kwa mtu mmoja mmoja, watumishi au taasisi zinazofanya vizuri zaidi katika utekelezaji majukumu yao, tuzo hizi zitawaongezea motisha ya kufanya vizuri zaidi.



Powered by Blogger.