MIL 360 ZA BAKAA KUTEKELEZA MIRADI VIPORO MANISPAA TABORA

 





Na Allan Kitwe, Tabora


MADIWANI wa halmashauri ya manispaa ya Tabora wameazimia fedha zote zilizotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026 na hazikutumika (bakaa) zisirudishwe TAMISEMI bali zitumike kukamilisha miradi viporo.


Hayo yamebainishwa na Katibu wa Madiwani wa CCM Bahati Adam Ntiruhungwa (diwani wa Kata ya Ng’ambo) alipokuwa akitoa maazimio yao kwenye kikao cha robo ya nne ya baraza kilichoketi leo Mjini hapa.



Ameeleza kuwa madiwani ndio wawakilishi wa wananchi katika Kata zao, hivyo wana dhamana ya kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao inakamilika kwa wakati kwa manufaa ya wananchi.


‘Madiwani wa CCM tumeazimia miradi viporo yote ikamilishwe, na fedha za bakaa, zaidi ya shilingi milioni 364 ziombewe kibali ili zitumike kumalizia miradi iliyoanza kutekelezwa katika msimu uliopita’, amebainisha.




Ntiruhungwa ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha wakazi wa kata zote wananufaika na juhudi za serikali yao za kuwaletea maendeleo kwa kuweka uwiano sawa wa miradi inayotekelezwa katika halmashauri hiyo.


Akifafanua zaidi, Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo Dkt John Pima ameeleza kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na madiwani wameyazingatia, na kubainisha kuwa wamepata baraka za TAMISEMI kutumia fedha za bakaa kwenye miradi.


Amewahakikishia kuwa wataendelea kuwa na usawazo mzuri wa miradi inayotekelezwa katika Kata zote na kuitengea bajeti ili kuboresha huduma za wananchi katika maeneo yote, hakuna Kata itakayoachwa nyuma.


Akitoa salamu za Mkoa, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa, Shani Mangesho, ameitaka halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kuharakisha utekelezaji miradi ya maendeleo na kukamilishwa miradi viporo.


Aidha amepongeza utaratibu mzuri wa uendeshaji vikao vya baraza katika manispaa hiyo kwa kuwa vinazingatia muda na kutanguliza maslahi ya wananchi.



Powered by Blogger.