RC MALISA AWASILI TABORA, AANZA NA USAFI

 




Na Mwandishi wetu, Tabora


ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Benno Malisa ambaye sasa amehamishiwa Mkoani Tabora amewasili Mkoani humo rasmi kuanza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi na kuahidi kusimamia kwa dhati suala la usafi.


Akiongea kwenye hafla maalumu ya mapokezi na kumuaga mtangulizi wake Paulo Matiko Chacha ambaye ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Oganaizesheni, ameeleza wazi kuwa ataendeleza mazuri yote.




RC Malisa amewashukuru Viongozi, Watumishi na wakazi wote wa Mkoa huo kwa mapokezi mazuri na kuahidi kuwa ataendelea kudumisha umoja na mshikamano uliojengwa na watangulizi wake na kusimamia mazuri yote.


Amedokeza kuwa Mkoa huo umepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na usimamizi mzuri wa Viongozi na Watumishi kwa kushirikiana na wananchi wote hivyo akaahidi kuwa ataendeleza mshikamano huo ili kufanya makubwa zaidi.


Amesisitiza kuwa wakati wa uapisho wa Wakuu wa Mikoa, Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliagiza wakasimamie ipasavyo suala la usafi katika Mikoa yao, na kuahidi kuwa atalisimamia kwa dhati, hivyo akaomba ushirikiano.


Kuhusu mvua za el nino, amesema kuwa Rais ameelekeza kila Mkuu wa Mkoa akajipange vizuri ili kuhakikisha mvua hizo hazileti madhara makubwa kwa wananchi na ikiwezekana wazuie ili zisilete madhara kabisa.


 ‘Katika hili, nawaombeni sana ndugu zangu, Wakuu wa Wilaya, Wataalamu na Watendaji wote tushikamane na tushirikiane kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa salama na mvua hizi hazileti madhara yoyote’, ameeleza.


Aidha amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo na Wakuu wa Wilaya kuweka mikakati thabiti ya kuongeza mapato katika maeneo yao na kusisitiza ushuru ulipwe kwa usahihi.


Awali mtangulizi wake, Paul Matiko Chacha amewashukuru wakazi wa Mkoa huo kwa ushirikiano waliompa alipokuwa Mkuu wa Mkoa na kuwataka wampe ushirikiano kama huo Mkuu wao mpya ili kazi iendelee.


Amemhakikishia RC Malisa kuwa Tabora ni mahali pazuri pa kufanyia kazi, wananchi wake ni wachapa kazi na asilimia 90 ya wakazi wote ni wakulima na kati ya hao asilimia 70 wanalima tumbaku ambayo haihitaji kusukumwa na mtu.


Amewaasa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma zaidi ili kuinua maisha yao na kulinda amani ya Mkoa huo na nchi kwa ujumla.


Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Said Juma Nkumba ameeleza kuwa ujio wa RC Malisa katika Mkoa huo unaleta faraja kubwa kwa wananchi kutokana na rekodi nzuri ya utendaji wake kule alikokuwa hivyo akamtaka kuendeleza rekodi hiyo.



Powered by Blogger.