VIONGOZI WA SMZ WATINGA KIBASILA KUJIFUNZA SIRI YA UFAULU WA 100%

 



Na Mwandishi Wetu


SHULE ya Sekondari Kibasila pamoja na uongozi mzima wa Shule hiyo umetoa pongezi za thati kwa Ziara ya Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) waliofika

Shuleni hapo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali lakini kubwa zaidi likiwa ni kujifunza juu ya mfumo mzima wa elimu ili na wao wakaboreshe mifumo yao ya Elimu huko Zanzibar.




Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam Dkt. Juma Boniface Orenda akisoma hotuba 

mbele ya wageni hao alisema, uongozi umefarijika na ujio huo mkubwa katika Shule yake.


Alisema hakika Shule hiyo ya Kibasila imekuwa ikijitahidi kwa asilimia kubwa kuboresha na kuweka mifumo imara na dhabiti ya utoaji elimu kwa wanafunzi wote kwa kushirikiana na mamlaka kuu ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka kwa kiwango cha juu.


" Kwa sasa watoto wetu wako kwenye ufaulu wa kiwango cha hali ya juu zaidi ambapo wanafaulu kwa asilimia 100 na hii ni 2024 kwenda 2025 tunaamini kadri tunavyozidi kusonga mbele ufaulu utakuwa wa ajabu zaidi," alisema Dkt. Orenda.


Aidha, alisema kuwa vile vile wanafunzi hao wamekuwa wakipatiwa vyeti viwili ambapo kwa wale wanaoshindwa kuendelea na masomo ya juu basi wanaendelea na masomo ya veta na hivyo kuendelea kufanya shughuli ambazo mwisho wa siku wanajiingizia kipato na kusema kuwa zipo hata suti, shati hadi suluali ambazo zimekuwa zikishonwa na wanafunzi wahitimu.


Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali ya Baraza la Wawakilishi Kombo Mwinyi Shehe, alitoa pongezi kubwa kwa Shule hiyo na kusema kuwa wameona kuwa upo umuhimu kwa kufika Shuleni hapo na kujifunza kuhusiana na mfumo mzima wa elimu na kusema kuwa kwa yale waliyoyaona hapo ikiwemo mpangilio wa masomo, walimu, madarasa, miundombinu mbalimbali ya ufundishaji na mambo mengine hakika wameondoka na jambo kubwa na wanaenda kulifanyia Kazi.


"Lakini tunatakiwa kujua jambo moja kwamba sisi ni wamoja na mambo yetu yanatakiwa kuwa mamoja ndio maana leo tumefanya Ziara Kibasila nasisi tunaenda kujipanga ili na nyie mfanye ziara Zanzibar na hii ni katika kuangalia jinsi tutakavyokuza kiwango chetu cha elimu kwa watoto wetu," alisema Mwenyekiti Shehe.


Viongozi mbalimbali walikuwepo kwenye ziara hiyo kutoka SMZ akiwemo Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu Pemba, Mohamed Nassor Sali pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Maadili Zanzibar Khadija Sulum Ali.


Mwenyekiti Kamati ya Ustawi wa Jamii Baraza la Wawakilishi Hussen Ibrahim Makungu, alisema"kwanza nimeshangazwa sana na ufaulu mkubwa kiasi hili hivyo kwa dhati nipende kuwapongeza sana na karibuni sana Zanzibar.


"Lakini kwa ufaulu huu ninahakika kuwa hata Wazazi hawajawatupa mkono bali na wao ni wadau wakubwa katika malezi na kuhakikisha watoto wanafanya vizuri mashuleni na majumbani lakini hata hii taarifa ya masomo mengine ya veta kama kushona na mengine nayo ni ya msingi zaidi,"alisema. 


Viongozi hao pia waliuliza maswala mbalimbali yanayohusu taaluma, viwango vya fedha zinazojenga mabweni ya wanafunzi kwani hivi sasa Kuna ujenzi wa mabweni ya wavulana, idadi ya walimu na wanafunzi, vitendea kazi vya kidigitali lakini juu ya watoto ambao wanashindwa kwenda kidato cha tano na sita na mambo mengine ambapo majibu yaliweza kutolewa papo hapo na Dkt. Orenda.


Lakini mmoja wa viongozi hao alihoji kuwepo kwa lugha ya kifaransa ambapo alielezwa kuwa lugha ya kingereza, kiswahili na kifaransakwa sasa hayana shida hata kidogo na hivi sasa wako kwenye mchakato wa kuwa na mwalimu wa lugha ya kijerumani huku taarifa ikiwema kuwa amali siyo somo la ziada bali lipo na ni mkombozi. 



Powered by Blogger.