ZAHANATI KALIUA YATOA HUDUMA MASAA 24

 




Na Mwandishi wetu, Kaliua                                                      


WAKAZI wa Kijiji Cha Zugimlole, Kata ya Zugimlole katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora wameeleza kufurahishwa na maboresho ya miundombinu ya Zahanati ya Kijiji hali iliyopelekea huduma kutolewa masaa 24.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa hali ya utoaji huduma katika Kata hiyo ilikuwa hafifu kutokana na kuchakaa miundombinu ya Zahanati hiyo kongwe, hali iliyopelekea akinamama kujifungulia nyumbani kwao.


Mariamu Nzumbe (50) mjasiriamali mkazi wa Kijiji hicho amepongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha huduma katika zahanati hiyo ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu akinamama kufuata huduma hizo katika Vijiji vingine.




‘Kwa sasa tunapata huduma zote hapa hapa tofauti na huko nyuma, hata watoa huduma sasa hivi wanaishi karibu na zahanati hivyo mjamzito akipata uchungu hata usiku anapatiwa huduma mara moja, tunahudumiwa masaa 24’, ameeleza.


Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo Dkt Anna Leonard Maghway ameishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi na miundombinu ya zahanati hiyo.


Ametaja maboresho yaliyofanyika kuwa ni kujengwa nyumba mpya ya watumishi (two in one), kuboreshwa miundombinu na kuongezwa watumishi, ambapo sasa kuna watumishi wa kudumu 3, wa mkataba 2 na wa ngazi ya jamii 3.




‘Maboresho haya yamewezesha wakazi wa Kata hii na maeneo jirani kuanza kupata huduma za afya kwa masaa 24, hali iliyosaidia kupunguza malalamiko ya wananchi ya kukosa huduma nzuri kwa muda mrefu’, ameongeza. 


Dkt Anna ameongeza kuwa katika maboresho hayo walitumia kiasi cha shilingi milioni 53.4 na kubakiwa na kiasi cha shilingi milioni 7.01 ambazo zitatumika  kukarabati majengo ya zahanati hiyo ili kuwa na mazingira bora zaidi.




Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Gerald Mongella amepongeza juhudi za dhati zinazoendelea kufanywa na serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu ya afya katika zahanati na hospitali zote Wilayani humo.



Powered by Blogger.