ZAIDI YA VIJANA 1,124 WAKUTANA KUJENGEWA UWEZO TABORA
Na Mwandishi Wetu, Tabora.
ZAIDI ya vijana 1,124 kutoka kata mbalimbali za Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wamekutana kwa siku mbili katika kongamano la kujengewa uwezo wa kiuchumi na kutambua fursa mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuchangia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kongamano hilo limewakutanisha vijana hao kwa ajili ya kupata elimu kuhusu utunzaji na matumizi sahihi ya fedha, fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, ujasiriamali, maadili, uzalendo pamoja na umuhimu wa kulinda amani na usalama wa nchi.
Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amewataka vijana kuzingatia elimu wanayopewa na kuitumia kujenga maisha yao, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa wazalendo, kulinda maadili na kushiriki katika kudumisha amani na usalama wa nchi.
Afisa Maendeleo wa Manispaa ya Tabora, Tumain Mgaya, amesema kongamano hilo limelenga kuwaongezea vijana uelewa kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi na kuwajengea uwezo wa kuzitumia katika kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji.
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo Hamza Murishid na Aisha Anthony wamesema wamepata elimu itakayowasaidia kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao na kuzitumia kwa ajili ya kujiletea maendeleo, huku wakiahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa na wawezeshaji.
Kongamano hilo pia ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kupokelewa Septemba 21, 2026 katika Wilaya ya Tabora, ambapo vijana hao wanatarajiwa kuwa miongoni mwa makundi yatakayoshiriki katika shughuli mbalimbali za mapokezi hayo.



