ASKOFU MKUU TAG ACHANGIA MIL 10 UJENZI KANISA LA KCC

 



Na Mwandishi wetu, Tabora


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la TAG Dkt Barnabas Mtokambali amechangia kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kitete Christian Centre (KCC) la Mjini Tabora ambalo ni Makao Makuu ya Jimbo jipya la Tabora Kati.


Askofu Mkuu ameahidi kutoa mchango huo kwenye ibada maalumu ya uzinduzi wa Jimbo jipya la Tabora Kati lililopo Mjini Tabora baada ya kufurahishwa na kazi nzuri ya ujenzi wa kanisa hilo la kisasa linalojengwa na Kanisa la KCC.




Ameeleza kuwa kanisa linalojengwa kwenye Makao Makuu hayo ya Jimbo jipya ni la kiwango cha juu, linavutia sana, hivyo akaahidi kuwaunga mkono ili kufanikisha maono hayo ya kujengwa kanisa la kisasa ambalo sasa limefikia asilimia 70.


Dkt Mtokambali amebainisha kuwa jengo hilo litaleta heshima kwa TAG na kuheshimisha Makao Makuu wa Jimbo ambayo yamezinduliwa rasmi katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na Viongozi wa serikali, Maaskofu, wachungaji na waumini.  


‘Nawapongeza sana wana KCC kwa maono haya ya kujenga jengo zuri na la kisasa la kuabudia, kanisa hili linampa utukufu Mungu, na mimi nitawasaidia shilingi milioni 10 ili kufanikisha kazi yenu hii’, ameeleza Askofu Dkt Mtokambali.



Amesisitiza kuwa Jimbo hilo ni tunda la kazi njema na  iliyotukuka iliyofanywa na watumishi wa Mungu, hivyo kipekee akampongeza Askofu mpya wa Jimbo hilo Rev Paul Meivukie kwa kazi yake njema na ya unyenyekevu mkubwa.      


Askofu Mkuu amewashukuru Maaskofu, Wachungaji wa TAG na Makanisa mengine na waumini wote kwa kumwombea alipokuwa amelazwa nchini India, hivyo akawataka kuwasha Moto wa Roho Mtakatifu katika Jimbo hilo.




Akitoa salamu za serikali katika ibada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt Gerald Mongela amepongeza kazi njema inayofanywa na TAG hapa nchini katika kuhubiri neno la Mungu na kutoa huduma za kijamii.


Ameomba wana TAG wote kuendelea kuliombea taifa amani, utulivu na mshikamano na kumwombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwatumikia wananchi kwa ufanisi na weledi mkubwa.


Mwisho.

Powered by Blogger.