DSE YAREKODI UKUAJI MKUBWA WA SOKO LA HISA

 





Soko la Hisa la Dar es Salaam, DSE, limerekodi ongezeko kubwa la shughuli za soko katika robo ya tatu ya mwaka huu.

Mtaji wa soko umefikia Shilingi trilioni 40.6, huku thamani ya miamala ya hisa ikipanda kwa zaidi ya asilimia 231.



Soko la Hisa la Dar es Salaam limeendelea kuimarika katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, huku likirekodi ukuaji katika mtaji wa soko, faharisi za hisa na thamani ya miamala.


Takwimu hizo zimetolewa leo, Oktoba 5, 2026, katika mkutano na wanahabari uliofanyika katika makao ya DSE, Exchange Tower, NHC Morocco Square, jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imewasilishwa na Mkurugenzi wa Fedha wa DSE, Lucas Sinkala, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa soko hilo, akishirikiana na Afisa Mkuu wa Fedha, Peter Situmbeko Nalitolela.



Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi Septemba 30, 2026, kampuni 28 zilizoorodheshwa katika DSE zilikuwa na mtaji wa jumla wa Shilingi trilioni 40.6.





Hiyo ni ongezeko la asilimia 90.3, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 21.34 zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Kwa kampuni 22 za Kitanzania, mtaji wa soko umefikia Shilingi trilioni 28.10, kutoka Shilingi trilioni 13.55 mwaka jana.

Hilo ni ongezeko la asilimia 107.4.


NMB Bank inaendelea kuongoza kwa kuwa na mtaji mkubwa zaidi wa soko, wenye thamani ya Shilingi trilioni 10.35.

Inafuatiwa na CRDB Bank, yenye mtaji wa Shilingi trilioni 7.70.

Katika faharisi za soko, DSE All Share Index, au DSEI, imefikia alama 4,654.22.

Hii ni ongezeko la asilimia 86.9 kutoka alama 2,489.70 mwaka jana.

Faharisi ya Hisa za Tanzania, TSI, nayo imepanda hadi alama 10,339.85, kutoka alama 5,118.80.

Hiyo ni ongezeko la asilimia 80.88.

Kwa mujibu wa DSE, ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na utendaji mzuri wa kampuni za sekta ya benki, zikiwemo NMB Bank, CRDB Bank na KCB Bank.

Faharisi ya Sekta ya Benki, Fedha na Uwekezaji, BI, imeongezeka kwa kasi zaidi.

Imefikia alama 23,382.10, kutoka alama 9,245.90 mwaka jana.

Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 152.89.

Katika soko la dhamana, hatifungani za Serikali zilizoorodheshwa katika DSE zimefikia thamani ya Shilingi trilioni 33.47.

Hii ni ongezeko la asilimia 17.19, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 28.56 mwaka jana.


Thamani ya hatifungani na dhamana za Sukuk za kampuni binafsi na taasisi za umma zilizoorodheshwa kwa fedha za Tanzania imefikia Shilingi trilioni 1.741.

Hii ni ongezeko la asilimia 46.70.


Dhamana zilizoorodheshwa kwa fedha za kigeni zimefikia Dola za Marekani milioni 186.05, kutoka milioni 153.74 mwaka jana.

Hilo ni ongezeko la asilimia 21.02.


Kwa upande wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja, ETF, thamani ya mtaji wa bidhaa hizo imefikia Shilingi bilioni 238.

ETF ya kwanza katika DSE iliorodheshwa Oktoba 2025 kupitia Vertex ETF, ikiwa na thamani ya awali ya Shilingi bilioni 6.8.

MIAMALA YA HISSA YAPAA

Katika eneo la miamala, DSE imerekodi ongezeko kubwa la biashara ya hisa.

Thamani ya miamala ya hisa katika robo ya tatu imefikia Shilingi bilioni 824.08.


Hii ni ongezeko la zaidi ya asilimia 231, kutoka Shilingi bilioni 248.64 katika robo ya tatu ya mwaka jana.

Wastani wa biashara ya hisa kwa siku ulikuwa Shilingi bilioni 8.96.


Hali hiyo inaashiria kuongezeka kwa shughuli za biashara na ushiriki wa wawekezaji katika soko.

Kwa upande wa hatifungani, thamani ya miamala katika robo ya tatu imefikia Shilingi trilioni 1.419.


Kiwango hicho ni pungufu kwa asilimia 12 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 1.617 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Hata hivyo, katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka, thamani ya miamala ya hatifungani imeongezeka kwa asilimia 5.76.

Imefikia Shilingi trilioni 4.366, kutoka Shilingi trilioni 4.128 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Wakati huo huo, miamala ya ETF katika robo ya tatu imefikia Shilingi bilioni 28.7.

Hii ni mara ya kwanza bidhaa hiyo kuonekana katika takwimu za robo ya tatu, kwa kuwa haikuwepo katika soko katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Kwa ujumla, takwimu za robo ya tatu zinaonyesha kuimarika kwa Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Ukuaji wa mtaji wa soko, kupanda kwa faharisi za hisa, kuongezeka kwa miamala pamoja na kuibuka kwa bidhaa mpya kama ETF, kunaongeza wigo wa shughuli na fursa za uwekezaji katika soko la mitaji nchini.

Powered by Blogger.