JESCA KITAMBAA CHEUPE AZINDUA CHIMBO LA VIJANA BRANCH 2026





Na Mwandishi Wetu — Dar es Salaam


Mfanyabiashara na mjasiriamali maarufu jijini Dar es Salaam, Jessica Boniface Kikumbi, anayefahamika kwa jina la Jesca Kitambaa Cheupe, amezindua hafla ya Chimbo la Vijana Branch 2026, inayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, Oktoba 24 na 25, mwaka huu.


Hafla hiyo inalenga kuwaunganisha vijana na wananchi kwa ujumla kwa kuwapatia burudani, huduma mbalimbali za kijamii pamoja na elimu kuhusu fursa za kiuchumi zinazoweza kuwasaidia kuboresha maisha yao.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jesca, King kikiambaye ni mmiliki wa kumbi za burudani na baa za Kitambaa Cheupe nchini, amesema hafla hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali katika eneo moja, badala ya kutumia muda na gharama kutafuta huduma hizo katika maeneo tofauti.


Amesema jukwaa hilo pia litatoa nafasi kwa vijana kupata elimu kuhusu ajira, uwekezaji, kodi na maendeleo ya kijamii, ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kila siku na mipango yao ya kiuchumi.


Kwa mujibu wa Jesca, hafla hiyo itaambatana na burudani kutoka kwa ma-DJ mbalimbali pamoja na wasanii watakaotumbuiza washiriki katika siku zote mbili za tukio hilo.


Aidha, washiriki watanufaika na huduma ya supu ya bure kuanzia asubuhi, ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizopangwa kuwakaribisha wananchi na kuongeza ushiriki wao katika hafla hiyo.


Mbali na burudani, Chimbo la Vijana Branch 2026 imewakutanisha watoa huduma na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya kijamii, kisheria, kifedha na kiuchumi, kwa lengo la kuwafikishia wananchi huduma na taarifa muhimu katika eneo moja.


Miongoni mwa taasisi zinazotarajiwa kushiriki ni Bodi ya Mikopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), pamoja na Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani.


Taasisi za bima na watoa huduma za afya pia wanatarajiwa kushiriki katika kutoa huduma na elimu kwa wananchi, huku taasisi zinazohusika na uwekezaji zikitoa ufafanuzi kuhusu fursa zilizopo na namna zinavyoweza kutumiwa kujiletea maendeleo.


Kupitia ushiriki wa taasisi hizo, wananchi watapata nafasi ya kuuliza maswali, kupata ufafanuzi kuhusu taratibu mbalimbali na kufahamu huduma zinazotolewa, pamoja na masharti ya kuzifikia.


Elimu kuhusu kodi, ajira, bima na uwekezaji inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya hafla hiyo, hususan kwa vijana wanaotaka kuanzisha au kukuza shughuli zao za kiuchumi.


Jukwaa hilo pia linatarajiwa kutoa nafasi kwa vijana kukutana, kubadilishana mawazo na kujenga mahusiano yanayoweza kuwasaidia katika shughuli za ujasiriamali na maendeleo ya kijamii.


Kwa ujumla, Chimbo la Vijana Branch 2026 inalenga kuunganisha burudani, elimu na huduma za kijamii katika jukwaa moja, huku ikiwapa vijana na wananchi fursa ya kufahamu huduma zinazopatikana na fursa zinazoweza kuchangia maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

Powered by Blogger.