STAMICO YAPATA MAFANIKIO MAKUBWA: MAPATO KUFIKIA TSH BILIONI 147.8 KUTOKA BILION 1.3

 





Na Mwandishi wetu-Dar es salaam


SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limepiga hatua kubwa kiutendaji na kifedha, likiongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 1.3 kwa mwaka hadi kufikia Sh bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/2026, kufuatia mabadiliko ya kimkakati na uwekezaji katika miradi mbalimbali ya madini nchini.


Mafanikio hayo yanaashiria mabadiliko makubwa ya shirika hilo, ambalo kwa miaka ya nyuma lilikuwa katika hali ngumu ya kifedha na kutegemea kwa kiwango kikubwa fedha za Serikali kuendesha shughuli zake, ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi.


Hayo yamebainishwa leo Oktoba 16,2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. CPA Venance Mwasse wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari nakusema kuwa mageuzi ya kuimarisha shirika hilo yaliyoanza mwaka 2020 yameimarisha uwezo wa shirika kujiendesha na kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali.


"Utendaji wa STAMICO umeweza kuongeza mapato yake kwa zaidi ya asilimia 11,000, hatua inayoonyesha kuimarika kwa uwezo wake wa kiutendaji na usimamizi wa miradi ya madini"amesema Mkurugenzi az


Dkt.Mwasse ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa watumishi kutoka 111 hadi karibu 800, kuingia mikataba minne ya ubia katika miradi ya madini ya kimkakati na kuendelea kuboresha mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Songwe.


Akizungumzia kuhusu wachimbaji wadogo, amesema shirika limeongeza mitambo ya uchorongaji kutoka mitatu hadi 18 na kuweka mitambo 17 kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji, sambamba na kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu.




"STAMICO ina masoko 44 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini takribani 120, vinavyorahisisha uuzaji rasmi wa madini na kusaidia kupunguza utoroshaji."amesema


Halikadhalika ameongeza kuwa mchakato wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji Tanzania umeanza kwa kushirikiana na wadau, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji wadogo.


Dkt. Mwasse amesisitiza kuwa STAMICO ni mwekezaji katika sekta ya madini, si mdhibiti, jukumu linalotekelezwa na taasisi husika za Serikali.




Aidha, shirika hilo linatekeleza na kushiriki katika miradi mbalimbali ya madini, ikiwemo mgodi wa dhahabu wa Stamigold, mgodi wa Buckreef uliopo mkoani Geita unaotekelezwa kwa ubia na kampuni ya Canada, pamoja na miradi ya nikeli, dhahabu, grafaiti na shaba katika maeneo mbalimbali nchini.




Miradi mingine iliyotajwa ni pamoja na mradi wa nikeli unaohusishwa na maeneo ya Nachingwea na Mlandizi, mradi wa dhahabu wa Kigosia, grafaiti ya Mererani na mradi wa shaba unaopatikana Mwanga.




Uwekezaji huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa, kuongeza mapato ya Serikali na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania.


Kwa upande Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mafanikio ya STAMICO yanaonyesha umuhimu wa mageuzi katika taasisi za umma, huku akisisitiza haja ya kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za kisasa ili kupima matokeo ya shughuli zake kwa usahihi.


Kumbuka kuwa STAMICO, ilianzishwa mwaka 1972 na inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100,inashiriki katika mnyororo wa thamani wa madini kuanzia utafiti na uchimbaji hadi uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini.

Powered by Blogger.