MANISPAA TABORA KUBORESHA MIJI YA PEMBEZONI YOTE

 




Na Allan Kitwe, Tabora


HALMASHAURI ya Manispaa Tabora iko mbioni kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya Miji/Mitaa ya Kata zote zilizoko pembezoni ili kupendezesha maeneo hayo na kuharakisha maendeleo ya wananchi.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Dkt John Marco Pima alipokuwa akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za maendeleo zilizotolewa na Waheshimiwa Madiwani.




Amesema kuwa halmashauri imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maeneo yote yaliyo katikati ya Mji na pembezoni ikiwemo maeneo yaliyorasimishwa.




‘Zoezi hili ni endelevu, tutaendelea kutenga bajeti ili kuhakikisha Mitaa yote inakuwa na miundombinu rafiki ya utoaji huduma za kijamii na huduma zinapatikana wakati wote’, ameeleza.


‘Nawapongeza wakazi wa Miji ya pembezoni kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa Viongozi wa Mitaa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, ushirikiano huu naomba uendelee kwa manufaa yenu’, ameongeza.


Awali diwani wa Viti Maalumu kupitia CCM, Halima Killa na Salum Msamazi wa Kata ya Ikomwa wamehoji mikakati ya Halmashauri kuboresha miundombinu ya Miji iliyoko pembezoni mwa manispaa hiyo ili kuondoa kero za wananchi.


Aidha wameeleza kusikitishwa na baadhi ya barabara kutopitika licha ya kuwepo ndani ya manispaa huku zingine zikitekelezwa na wakandarasi kwa muda mrefu hali iliyopelekea kulalamikiwa na wananchi.


Katika hili Mkurugenzi, Dkt Pima ameeleza kuwa wameunda Kamati Maalumu ya Maafa ambayo inapita katika Kata zote zilizopo katikati ya Mji na pembezoni mwa Mji ili kuangalia changamoto zilizopo na kuzishughulikia haraka iwezekanavyo.


‘Kamati hii ni ya muhimu sana kwani itasaidia kubaini maeneo korofi yote na kushauri nini kifanyike ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza punde mvua kubwa za el nino zitakapoanza kunyesha, katika hili tumejipanga vizuri’, ameongeza.


Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ghullam-Hussein Dewj ambaye pia ni diwani wa Kata ya Kanyenye amepongeza mikakati mizuri ya halmashauri kuboresha miundombinu ya Miji ya pembezoni kwa kuwa itaharakisha maendeleo.


Aidha amemtaka kuhakikisha Kamati ya Maafa inatengewa bajeti ya kutosha hasa katika kipindi hiki ambacho mvua za el nino zinatarajiwa kuanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ili kuepusha maafa kwa wananchi.


Mwisho

Powered by Blogger.